HEDHI – Kikwazo cha Elimu kwa Baadhi ya Mabinti

Kuna sababu nyingi zinazopelekea mabinti katika nchi zinazoendelea kutokuendelea na elimu ya sekondari au kutokumaliza elimu ya sekondari.

 

Kitu kikubwa kinachowafananisha wanawake wote duniani ni suala la hedhi anayopata mwanamke kila mwezi. Mwanamke hupata hedhi kwa wastani wa miaka arobaini. Katika kipindi chote cha miaka arobaini mwanamke anaweza kutumia Vihifadhi Hedhi (pads) Zaidi ya 11,000 ambazo inambidi anunue.

Kwa mwanamke ambaye kipato chake ni cha kutosheleza mlo mmoja tu kwa siku – hawa wapo zaidi katika chini zinazoendelea kama Tanzania – hedhi yake ya kila mwezi inaweza kuwa ni moja kati ya changamoto kubwa anazokutana nazo katika maisha yake. Kwa binti anayeishi katika familia ambayo kipato chake ni cha kutosheleza angalau mlo mmoja tu kwa siku, hedhi yake ya mwezi inaweza kumuathiri sana uwezo wake wa kuhudhuria shule na hivyo kuweka njia panda hatma ya fursa yake ya kupata elimu. Mabinti wengi wanashindwa kuhudhuria masomo wanapokuwa katika hedhi kutokana na ukosefu wa vihifadhi hedhi kwani wanahofia kuchafuka jambo ambalo litapelekea kudhihakiwa na wanafunzi wenzao hasa vijana wa kiume.

 

Uwezekano wa mabinti katika nchi zinazoendelea kupata elimu bora upo endapo tu pamoja na jitahada nyingine, watatengenezewa mazingira mazuri ya kujisitiri hasa wanapokuwa katika mzunguko wao wa hedhi. Mazingira hayo ni kujengewa maliwato ambazo zitakuwa na sehemu maalumu za kujisafisha na kujisitiri, yaani kubadilisha kihifadhi hedhi pindi binti anapokuwa kwenye mzunguko wake wa kila mwezi.

 

Ukifuatilia utaona kwamba maeneo ya vijini ambako ndipo walipo wanannchi wengi, idadi ya watoto wa kike wanaojiunga na elimu ya msingi ni kubwa ukilinganisha na idadi ya wanaojiunga na elimu ya sekondari. Moja kati ya sababu ni mabinti wengi kuvunja ungo baada ya kumaliza darasa la saba. Kwa mabinti ambao wametoka familia zenye uchumi mdogo kwani familia haimudu gharama za vihifadhi hedhi, na hawako tayari kuona binti yao akidhalilika akiwa shuleni punde hali hiyo inapotokea – moja ya hofu ya wazazi mabinti ni zao kuweza kubakwa na wanafunzi wenzao, vijana wa mitaani au hata walimu wao.   Uelewa mdogo wa wazazi kuhusu hedhi huwafanya waamini kwamba mtoto wa kike akishavunja ungo anatakiwa kuzaa na si vinginevyo, na njia pekee ni kumuozesha ili asije kupata ujauzito akiwa bado chini ya himaya yao.

 

Kwa muda mrefu wadau wengi wa masuala ya elimu wamekuwa wakiamini kwamba ni rahisi binti kuacha shule akiwa akiwa ameshika ujauzito au kuolewa. Kwa miaka ya hivi karibuni hii imekuwa tofauti kwani, mabinti wasiokuwepo mashuleni ndio wanaopata mimba zisizotarajiwa na wengine kuolewa katika umri mdogo.

 

Wafadhili, Watungaji wa Sera za Elimu na wadau wengine wa elimu bado wanaamini kwenye manufaa atakayopata binti kwa muda mrefu baadaye endapo atapata elimu sahihi, ambayo ni ajira nzuri. Kiwango kidogo cha mkazo au msisitizo kimewekwa kwenye manufaa anayoweza kupata binti kipindi anachokuwa anasoma hasa akiwa katika elimu ya sekondari kama vile kujitambua, kuepuka mimba za utotoni, kuolewa kabla ya umri sahihi, nk

 

Ubinti ni changamoto kwa kuwa ni kipindi ambacho binti anatakiwa kupata elimu lakini wakati huo huo kuna vitu vingine vinavutiwa na umri aliofikia kama vile hisia za mapenzi na kushiriki tendo la ndoa; majukumu ya kusaidia kazi za nyumbani yanaongezeka, wakati mwingine anaanza kubeba majukumu ya familia, nk Kila jambo kati ya hayo yaliyotajwa hapo juu lina athari kwa upatikanaji wa elimu bora kwa binti kwa namna moja au nyingine. Hali hii ina athari kubwa zaidi kwa mabinti wanaoishi vijijini ambao maisha yao bado yamefungwa zaidi kwenye mila na desturi kama vile ndoa za kulazimishwa, mimba zisizotarajiwa, kubakwa na kupata watoto katika umri mdogo.

 

Ikumbukwe pia kwamba, ni katika kipindi cha mwanadamu kubalehe ambapo tofauti za majukumu kati ya mtoto wa kike na wa kiume zinapoonekana zaidi kwani ni katika matayarisho ya kuingia kwenye utu uzima. Hiki ni kipindi ambacho elimu ndio kitu kipekee kinachoweza kumsaidia binti kujitambua na kutambua nafasi yake katika jamii ili kuweza kumudu changamoto za kijami, kutoharakisha kufanya maamuzi ya kubeba majukumu ya familia kama vile kuolewa na kupata watoto, kumjengea uwezo wa kina wa namna anavyoweza kuyamudu maisha yake na kusaidia jamii. Kwa bahati mbaya mabinti walio wengi hawapati fursa hii.

 

 

Save

1 reply
  1. lornadf
    lornadf says:

    Thank you for visiting. Your comment means a lot to us. Let us do it for the Girls! Four our nation! For the World! For Love!

    Reply

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply to lornadf Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *