NISITIRI DHAMINI HEDHI CAMPAIGN: MCHINGA EXPERIENCE – PHASE II

MIPINGO SECONDARY SCHOOL, LINDI TANZANIA

Oktoba 2021 tulitembelea shule nne za sekondari Wilayani Lindi katika jimbo la Kisiasa la Mchinga. Tuliweza kuwafikia mabinti 584 kwenye shule hizo kwa kuwapatia elimu ya makuzi, afya ya uzazi na afya ya hedhi. Pamoja na kutoa elimu hiyo, tuliwapatia pia zawadi za taulo za kike za kufua kwa ajili ya kujisitiri wakati wanapokuwa katika hedhi ya mwezi; Nisitiri Reusable Sanitary Pads

Beautiful girls of Mipingo Secondary School, Lindi – Tanzania
Madam Lorna explaining how to use and care Nisitiri Reusable Sanitary Pads to Mipingo Secondary school girls
Mr. Naseem offering reproductive health education to Mipingo Secondary School girls
Madam Sheila offering Menstrual Hygiene and Health management education to Mipingo Secondary School girls
Some of Mipingo Secondary School girls with their Nisitiri Reusable Pads gifts
Liquid absorption test

NISITIRI DHAMINI HEDHI CAMPAIGN – Mchinga Experience

Tarehe 09.12.2020 kulikuwa na Kongamano la Wasichana kwenye ukumbi uliopo katika jengo la Jubilee Tower, jijini Dar es Salaam. Ni moja kati ya makongamano ya wanawake ambayo yalikuwa na mvuto mkubwa sana. Timu ya #NisitiriDhaminiHedhi kampeni ilishiriki kongamano hili pia.

09.12.2020 Nisitiri Dhamini Hedhi campaign awareness

Mh. Salma Kikwete alikuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo. Baada ya kongamano kama ilivyo ada, alitembelea meza za wafanyabiashara mbalimbali waliokuwa nje ya ukumbi huo. Tulikuwa na meza kwa ajili ya #NisitiriReusablePads. Hatukuchukua meza kwa ajili ya biashara bali kwa ajili ya kuelemisha watu kuhusu changamoto wanayokutana nayo mabinti kutoka familia maskini wanapokuwa katika siku zao za hedhi.

Hon. Mama Salma Kikwete explaining something to LDF Member on 09.12.2020

Mama, Mh. Salma Kikwete aliziona taulo za kike za #Nisitiri na tukamwelimisha japo kwa ufupi ni namna gani zinaweza kumsaidia mtoto wa kike hasa kutoka familia yenye changamoto ya kiuchumi.  Alizifurahia na akatufahamisha kuhusu changamoto zilizopo katika jimbo la Mchinga.  Baada ya kutueleza akatukaribisha pia Mchinga ili tukajionee wenyewe na kuweza kuwasaidia mabinti wa eneo lile.

Tarehe 22.02.2021 tulipata neema na kibali kutoka kwa MUNGU kuweza kufika Manispaa ya Mchinga, wilayani Lindi katika mkoa wa Lindi. Tulipokelewa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mchinga, ofisi ya Mbunge wa Mchinga na mwakilishi wa WAMA Foundation (Taasisi isiyo ya Serikali inayoongozwa na Mh. Mama Salma Kikwete).

Tulitembelea shule mbili za sekondari; Kitomanga na Milola. Tulipata nafasi ya kuzungumza na walimu na wanafunzi.  Changamoto ni kubwa sana sio tu upatikanaji wa taulo za kile bali pia elimu sahihi kuhusu hedhi.

#NisitiriReusablePads distribution to Kitomanga Secondary School girls

Katika kila shule tulitoa zawadi ya boksi mia moja za #NisitiriReusablePads kwa ajili ya wanafunzi wa kike mia moja.

#NisitiriReusablePads distribution to Milola Secondary School girls

Girls at Kitomanga Secondary School with their gift of #NisitiriReusablePads

Watu wa Mchinga ni wakarimu sana.  Mchinga imetawaliwa na kijani kibichi.  Hali ya hewa ni nzuri sana.  Tulishuhudia maembe na nazi zilizoanguliwa zikiwa katika malundo malundo kwenye makazi ya watu mbalimbali wakati tukiwa tunaelekea Milola. 

Mchinga ni pazuri sana.  Tutarudi tena.

NISITIRI DhaminiHedhi Campaign – Kyela, Mbeya

August, 2020 Nisitiri Reusable Pads ziliwafikia mabinti wa wilaya ya Kyela mkoani Mbeya
Nisitiri Reusable Pads Kyela, Mbeya reach out.

Ilikuwa ni furaha kubwa sana kuweza kuwafikia mabinti hamsini (50) katika wilaya ya Kyela mkoani Mbeya na kuwapatia taulo za kike za Nisitiri.

Mmoja wa mabinti hawa aliileza timu nzima ya Nisitiri Project kwamba taulo hizi ni msaada mkubwa sana kwake kwani kabla ya hapo amekuwa akitumia magodoro yaliyochakaa pindi anapokuwa katika siku zake za hedhi ya mwezi.

Nisitiri Dhamini Hedhi campaign ni kwa ajili ya kuwasaidia mabinti ambao wanatoka katika familia maskini. Familia masikini ambazo hazina uwezo hata wa kukidhi mlo mmoja kwa siku hivyo kufanya suala la kumnunulia binti taulo za kike za kujisitiri wakati wa hedhi kuonekana kama ni anasa.

Campaign hii inahusisha kila mtu mwenye mapenzi mema na mabinti. Hedhi ni fahari ya mwanamke yeyote kwani humpa uhakika kwamba anacho moja kati ya vigezo muhimu sana cha kumpa sifa na uwezo wa kuongeza mwanadamu mwingine duniani.

Nisitiri Reusable Pads zinatayarishwa na LornaDadi Foundation na kutolewa bure kwa wanaufaika, yaani mabinti wenye uhitaji. Gharama za kutayarisha pakti moja ambayo ina taulo nne za kike (sanitary pads) ni kiasi cha TZS. 12,000/- tu. Hatuna mfadhili yoyote rasmi kwa ajili ya project hii bali ni watu mbalimbali (mtu mmoja mmoja) hujitolea kwa kununua hizi pakti kwa kadri wanavyowiwa.

Ikiwa unaguswa na campaign hii tafadhali wasiliana nasi kupitia simu nambari +255 786 666866 au tuma barua pepe kwenda lornadadi@gmail.com

Tunazidi kuwafikia mabinti mbalimbali kutoka sehemu tofauti tofauti za Tanzania. Na siku si nyingi tutaanza kukuletea simulizi za maisha yao ya ubinti hususani changamoto wanazozipitia wakati wa hedhi kupitia youtube channel yetu.

Asante kwa kutembelea website yetu.

NISITIRI: Nina Vipande vya Maisha Vilivyopotea

Wanayopitia Mabinti katika Ubinti wao!

Maisha yangu yamejaa uchungu na aibu” ….. Batuli Mwinyiheri

“Ninatamani kuendelea na masomo lakini nashindwa kutokana na hali halisi ya maisha yangu na wazazi wangu.

Nina umri wa miaka 14, baba yangu mzazi alishafariki na mama yangu aliolewa na mwanaume mwingine. Mume wa mama yangu, yaani baba yangu anayenilea sasa amekuwa akinitesa japo kama hupitii ninachopitia huwezi kuamini kama ananitesa. Mbele za watu anaonekana kutujali mimi na mama lakini sivyo ilivyo katika maisha halisi tunayoishi nyumbani kama familia.

Mama yangu amekuwa dhaifu kiafya kwa muda wa miaka miwili sasa. Anasumbuliwa na mgongo kutokana na kupigwa na baba. Mimi ndiye nimekuwa nikimtunza mama hasa nyakati za mchana ambapo baba anakuwa amekwenda shambani.

Nimeshavunja ungo. Nikiwa katika siku zangu huwa ninapata maumivu makali sana ya tumbo, mgongo, kiuno na kichwa. Katika kipindi kama hiki, siwezi kuvuka kizingiti cha mlango kwa sababu damu inachuruzika sana na sina kitu cha kuweka ili isipitilize.

Nguo zangu zimechakaa zote hadi sasa navaa nguo za shule hata ninapokuwa nyumbani nikimuuguza mama.

Mimi ndiye nafanya kila kazi nyumbani. Naamka saa kumi na moja asubuhi ili nikateke maji, nirudi nichanje kuni, nisafishe uwanda wa nyumba, niandae kifungua kinywa. Nimuogeshe na kuhakikisha amekula vizuri.

Nikitaka chochote kutoka kwa baba hata kama ni kwa ajili ya chakula anasema ni lazima nilipie. Nikimwambia sina hela anafanya tendo la ndoa na mimi kwanza ndipo anipe ninachohitaji. Wakati mwingine ananifanyia hivyo na asinipe ninachohitaji. Mara nyingi ananiambia inabidi nimsaidie mama yangu kwani alimuoa kwa ajili hiyo. Sijawahi kumwambia mama kwani najua ataumia sana. Naona kabisa maisha yangu yanavyopotea.

Nakushukuru sana nimeongea na wewe. Naomba unisaidie mama yangu apone. Akipona nitafurahi sana. Mama akipona najua nitarudi shule. Lakini pia naomba unisaidie nipate vitambaa vya kuweka nikiwa kwenye siku zangu.”

Nisitiri – DhaminiHedhi Kampeni

Nisitiri – Dhamini Hedhi ni kampeni yenye lengo la kuwafikia mabinti elfu moja kutoka kwenye familia zenye changamoto ya kiuchmi kiasi cha kushindwa kutimiza hitaji la kununuliwa taulo za kike.

Lengo la kampeni hii ni kuwasitiri mabinti hawa wanapokuwa katika hedhi ya mwezi kwa kuwasaidia kupata taulo za kike.  Kama tunavyojua, mwanamke anapokuwa katika hedhi kuna damu inayokuwa inatoka kwenye mwili wake kupitia viungo vyake  za uzazi.  Katika kipindi hiki mwanamke anahitaji kuwa amesitirika ili kwamba ile damu inayotoka kipindi hicho isipitilize na kuonekana kwa nje na mtu mwingine.  Hedhi ni jambo la staha, damu inayotoka inapaswa kuonwa na anayetokwa damu tu na si vinginevyo.  Mwanamke au binti anahitaji taulo za kike kwa ajili ya kujisitiri katika kipindi hiki.

Hedhi ni jambo la asili.  Hedhi ni jambo la uumbaji lililofanywa na MUNGU mwenyewe.  Kila mwanamke aliye kamili huwa na vipindi vya hedhi baada tu ya kuvunja ungo. Hedhi sio jambo ambalo mtu anaweza kuchagua kuwa nayo au kutokuwa nayo.

Inapotokea kwamba, mwanamke au binti yeyote anashindwa kujisitiri katika kipindi hiki cha hedhi, maisha yake hujaa simanzi na unyonge; ujasiri wote humuishia kwani anakuwa katika hali ya mashaka kwamba huenda akachafuka muda wowote kwa damu inayokuwa ikimtoka mwilini mwake kupitia viungo vyake vya uzazi.  Hii damu inapotoka haitoi ishara ya namna yoyote kama vile unapokuwa unasikia haja ndogo au haja kubwa, hii hutoka tu.

Katika mazingira kama haya, binti anapokosa taulo za kike kwa ajili ya kujisitiri kwenye kipindi hiki cha hedhi inamwia vigumu sana kufanya jambo lolote ikiwemo kuhudhuria masomo.

  • Ili mwanafunzi ahudhurie ipasavyo masomo yake anatakiwa ahudhurie siku 194 na vipindi 1740 katika mwaka mmoja wa masomo.
  • Lakini kwa mtoto wa kike hasa wa kijijini amekuwa akikosa masomo kwa wastani wa siku 84 kwa mwaka kutokana na suala la hedhi ambalo ni suala la kimaumbile.
  • Jambo hilo humfanya msichana kukosa kuhudhuria vipindi 756 vyenye Dakika 40 kila kimoja.
  • Hii ni kutokana na changamoto ya kipato cha wazazi wao na pia shule nyingi nchini hasa za vijijini kutokuwa na mazingira rafiki ya usafi kwa wanafunzi wa kike.

Kupitia NISITIRI – Dhamini Hedhi kampeni tunaungana pamoja na serikali, mashirika mbalimbali na jamii kwa ujumla kuhakikisha mtoto wa kike anapata vihifadhi hedhi, yaani taulo za kike, kwa ajili ya kujisitiri katika mzunguko wake wa mwezi lakini pia anapata elimu na uelewa zaidi kuhusu Hedhi salama.

Lengo la kampeni hii ni kuwafikia mabinti elfu moja wanaokaa vijijini. Ni kampeni ya miezi mitano kuanzia 01.02.2020 hadi 30.06.2020. Paketi moja ya taulo za kike itamwezesha binti mmoja kuwa na uhakika wa kuishi bila hofu ya kutokusitirika wakati wa hedhi yake ya mwezi kwa muda wa miaka miwili. Paketi moja inapatikana kwa gharama ya TZS. 10,000/- . Aina ya taulo za kike tunazotegemea kuwapatia ni zile ambazo anaweza kuzifua baada ya kuzitumia. Unaweza kuchangia kupitia https://www.wezeshasasa.com/nisitiri-dhamini-hedhi

Kiwango chochote kuanzia shilingi 1,000/- za Kitanzania.

Asante sana. Karibu ushiriki kwenye kampeni hii yenye mashiko kwa maisha ya binti.