KUWA MWENYE FURAHA

Ni vizuri kuwa mwenye furaha! Je, unajua kuwa kuna njia nyingi unazoweza kujisaidia wewe mwenyewe kuwa mwenye furaha?

Hizi ni baadhi ya zile ambazo mimi huwa natumia kujisaidia kuwa mwenye furaha:

  1. Najitahidi kuimarisha uhusiano wangu na MUNGU nyakati zote: za vicheko ama vilio, raha ama huzuni, kukosa ama kupata, kupanda ama kushuka, nk.
  2. Kushughulisha akili yangu zaidi kwa mambo yanayoleta mtazamo chanya wa maisha
  3. Hupenda kuufanyisha mwili wako mazoezi, (nafanya mazoezi madogo madogo sana kwa wafanya mazoezi hawawezi kuyaita ya kwangu ni mazoezi).  Kufanya mazoezi huchangia sana kuwa na afya bora sio tu ya mwili bali na akili pia.
  4. Najitahidi kulala usingizi wenye utulivu. kwa watu wanaonijua wanasemaga “Lorna ana kifurushi cha kutosha cha usingizi”. Hii ni kwa sababu, linapokuja suala la kulala hata kama ni nusu saa tu mimi kwa kweli huwa nahakikisha nimelala. Na ninapolala akili yangu, moyo wangu, roho yangu na mwili wangu najitahidi sana viwe katika utulivu. Kuchoka sana kunaweza kuharibu hisia zako. Watu ambao hawana usingizi wa kutosha au hawapati usingizi tulivu wataalamu wanasema wapo kwenye hatari kubwa sana ya kupata tatizo la msongo wa mawazo.
  5. Najitahidi kupata mlo sahihi kwa wakati sahihi.  Mwili usipopata nguvu ya kutosha kwa kadri inavyohitajika kuna vitu havitaenda sawa katika mfumo mzima wa utendaji kazi wa mwili; hii huathiri hata uwezo au utendaji kazi wa akili ya mtu pia.
  6. Najitahidi kujenga mahusiano mazuri na watu tofauti kwa kadri ninavyokutana nao katika nyanja na hatua mbalimbali za maisha yangu. Naamini kwamba kuwa na mahusiano sahihi kunatengenezwa zaidi na kuwa na mawasiliano sahihi. Ninajitahidi kumweka kila mtu ninayekutana naye kwenye maisha yangu kwenye nafasi anayostahili kuwekwa na mimi ndani nyangu. Huwa nina akiba ya namna ninavyomchukulia mtu. Hii inanisaidia kujiepusha na vitu kama vile kumtarajia mtu awe wa aina fulani kwangu kumbe yeye kwangu mimi alivyojiweka ni tofauti na ninavyomchukulia.
  7. Ninalinda sana kile kilicho ndani yangu. Huwa siruhusu mtu yeyote aniburuze kwa namna yoyote ile; iwe hisia zangu, werevu wangu, nguvu zangu, maono yangu, moyo wangu au kitu kingine chochote kile ambacho kiuhalisia ni cha kwangu ambacho MUNGU ameweka ndani yangu. Huku Duniani kuna watu wanajua jinsi ya kurudisha watu wengine nyuma; anaweza kukufanya ukajihisi mjinga, huwezi kabisa kufanya chochote au ndoto uliyo nayo ni ujinga tu! Watu wa aina hii ukiwapa nafasi kwenye maisha yako ni rahisi sana kukubadilisha namna unavyofikiria kuhusu wewe mwenyewe. Unavyojifikiria kuhusu wewe mwenyewe ni nguzu muhimu sana ya maisha yako na kile kinachokwenda kudhihirika kwenye maisha yako. Ninaamini kwamba jinsi ninavyojisikia kujihusu na jinsi ninavyoamini kuhusu mimi mwenyewe huathiri sana mtazamo na imani yangu jinsi ninavyoamini kuhusu maisha na ninavyoyachukulia maisha kwa ujumla
  8. Ninatambua kwamba haijalishi nitafanya kitu chenye fedha nyingi kiasi gani au kunitanisha na watu maarufu kiasi gani au mimi mwenyewe kuwa maarufu kiasi gani, kama sitaishi maisha aliyonikusudia MUNGU kuishi hapa Duniani basi kamwe siwezi kuwa na furaha ya kweli maishani mwangu. Ninaamini kwamba, maisha yanayoweza kuni furaha ya kamili ni maisha ya kuziidhi ndoto zangu, maisha ya kuliishi kusudi la maisha yangu na maono MUNGU aliyoweka ndani yangu. Na nimechagua kukubali kwamba, jukumu la kutimiza maono yangu au ndoto zangu ni la kwangu mwenyewe.
  9. Siruhusu mtu yeyote yule au kitu chochote kile asimame au kisimame kama kikwazo cha mimi kutekeleza ninachopaswa kutekeleza ili kutimiza maono yangu. Na wala sihamishi jukumu la utekelezaji wa maono yangu au ndoto zangu kwa mtu mwingine yeyote yule.
  10. Ninaamini kwamba watu ambao MUNGU amewakusudia kuwa na mimi katika kutekeleza maono aliyoweka ndani yangu kwenye hatua tofauti tofauti za maono hayo, sio kila mtu ni sehemu ya ndoto au maono yangu haijalishi ni mtu wa karibu kwangu kiasi gani. Hii inanisaidi kuimarisha uhusiano wangu na watu wasionisapoti kwenye maono yangu.
  11. Naamini katika kusaidia weninge pale ninapoweza kufanya hivyo. Kusaidia watu wengine kunanipatia hisia za kusihi maisha yenye mguso kwa weninge hivyo kuniondolea kiburi cha kujiona mimi ni bora zaidi au ninastahili zaidi vitu fulani vya maisha kuliko kwengine. Ninaamini kwenye kutenda mema hapa Duniani.
  12. Najitahidi kuwa mwaminifu kwangu mwenyewe. Kwa kufanya hivi ninaweza kutimiza vitu vingi ambavyo nimejiwekea malengo mwenyewe. Nisipokuwa mwaminifu juu yangu au juu ya mambo yangu mwenyewe kamwe siwezi kuwa mwaminifu kwa watu wengine au mambo yanayohusu watu wengine.

Je ipo yoyote unayoona inakufaa katika ya hizo kumi na mbili?

Je, wewe unatumia njia gani au unafanya vitu gani kuhakikisha una furaha muda mwingi?

Niandikie hapo chini kwenye comment ili mimi na wengine tujifunze zaidi na kuboresha maisha yetu ya ndani.  Furaha ya kweli huboresha maisha yetu ya ndani.  Maisha yetu ya nje ni tafsiri ya maisha yetu ya ndani.

Andiko hili limepewa nguvu na kitabu cha Simulizi za “Vipande vya Maisha Vilivyopotea

MAFANIKIO YENYE USHAWISHI – II

ASILI YA MAFANIKIO

Katika mafanikio kuna vitu viwili ambavyo usipovielewa vinafanyaje kazi katika kuchangia wewe kupata mafanikio yako, utachanganyikiwa.  Vitu hivyo ni Sheria na Kanuni.

Fahamu:  Kuna sehemu ya Kanuni katika mafanikio au kutokufaniniwa kwa mtu binafsi na kuna sehemu ya sheria katika mafanikio au kutokufaniniwa kwa mtu binafsi.

Tofauti ya Sheria na Kanuni

Sheria zinaweza kukuzuia kufikia mafanikio unayotaka kuyafikia.  Yeyote anayetaka kufanikiwa ni lazima avunje sheria za maisha.  Kushindwa kwako katika maisha kunasababishwa na kitendo chako cha kuamua kuwa unatii sheria za maisha.  Usichanganye Sheria na Kanuni.

Kanuni za maisha

Kanuni za maisha hazifanyi kazi kulingana na kile ulichowahi kupitia katika maisha yako au unachopitia sasa, hapana.  Zinafanya kazi wakati wote, haijalishi kama unajua uwepo wa hizo kanuni au hujui.

Mafanikio yanatabirika na kushindwa pia kunatabirika kwa sababu kila kitu katika maisha kiliumbwa kufanya kazi kwa kanuni.  Kanuni huyafanya maisha kutabirika.  Kila kitu kina kanuni inayoambatana nacho kwa sababu kila alichoumba MUNGU kinapaswa kufanikiwa. Kila kitu kinafanikiwa kwa kufuata kanuni.  Kila mtu anafanikiwa kwa kufuata kanuni. 

MUNGU alimuumba mwanadamu kwa ustadi wa kiwango cha hali ya juu sana.  MUNGU aliweka kanuni ambazo endapo mwanadamu atazifuata ni lazima atafanikiwa.  Chochote alichokiumba MUNGU ni lazima kifanikiwe.  Mafanikio ni jambo zuri mbele za MUNGU.

Mafanikio ni muhimu.  Ukitaka kufanikiwa katika maisha usijaribu kufanikiwa katika maisha.  Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu wanajaribu kufanikiwa.  Watu waliofanikiwa hawakujaribu kufaninikiwa, walitekeleza kwa vitendo kanuni za mafanikio na kanuni za maisha.  Kwa maneno mengine, mafanikio ni matokea ya kuwa mtiifu kwenye kanuni.

Mafanikio ni matunda ya shughuli unayojihusisha nayo yaliyotokana na wewe kufuata kanuni.

Unajuaje kama umefanikiwa?

Mafanikio hayapimwi kwa kulinganisha jambo ulilofanya wewe na alilofanya mtu mwingine kwani siku zote wapo watu uliowazidi na waliokuzidi pia.  Mafanikio yanapimwa kwa kulinganisha kati ya kile ulichofanya na kile unachopaswa kufanya.  Mafanikio yanapimwa kupitia nia ya msingi ya wewe kufanya hicho unachofanya.  Mafanikio yako hayapimwi kutokana na kile ulichofanya, hapana, mafanikio yako hupimwa kutokana na lile kusudi la MUNGU kukuumba.  Mafanikio ni utimilifu wa kusudi la MUNGU juu ya maisha yako.  Mafanikio katika maisha yako yanachochewa na kusudi la MUNGU juu ya maisha yako, yaani kile kitu ambacho MUNGU alikuumba uje kukitimiza hapa duniani.  Mafanikio ni kutimia kwa mpango wa MUNGU juu ya maisha yako. Kuna kusudi MUNGU ameweka ndani yako na kuna mahali MUNGU anataka ufike. Haijalishi ni watu wangapi watakusifia, watakushangilia na kukupongeza, kama hukufanya kile kitu ambacho MUNGU anataka ufanye na kama hukufika pale ambapo MUNGU anapotaka ufike, wewe hujafanikiwa. Mafanikio ya Kiungu yanapimwa kwa kufikia ile hatima ambayo MUNGU amekukusudia.  Maisha sio kwa habari ya kufanya kazi kwa bidii lakini kufanya kazi kwa werevu na uhodari kwa kutumia maarifa sahihi.  Utaweza kufanya kazi kwa werevu ukiwa na maarifa yaliyofichwa kwenye kanuni. Chochote unachoanza kufanya au unachoacha kufanya kinategemea zaidi na kanuni unazozifuata au kutozifuata. Kufanikiwa kwako au kushindwa kwako kunategemea na kanuni za maisha unazotii au kutokutii.   Mafanikio sio suala la MUNGU bali ni juu yako wewe mwenyewe.

Mafanikio ni mchakato.  Mafanikio yanavutiwa zaidi na wewe kuwa unaenenda katika mwelekeo sahihi kuliko wewe kufika pale unapokwenda.  Mafanikio ni ule mchakato unaoupitia kuelekea kule unakotakiwa kufika na sio kufika kule unapotakiwa kufika.  Yaani mafanikio yanapatikana hapa njiani kwenye safari ya kuelekea kule unakotaka kufika.  Ukifanikiwa kwa kupitia mchakato sahihi unakuwa umetimiza kusudi lako.

Kama huzijui kanuni za hicho kitu unachotaka kufanikiwa ni dhahiri kwamba hutaweza kuzitii hizo kanuni, Unaposhindwa kuzitii hizo kanuni huwezi kufaninikiwa.  Haijalishi utajibidisha kwa kiwango gani au utamwomba MUNGU kwa kiasi gani.  Mafanikio ni matokea ya kutii kanuni.

Mafanikio yenye ushawishi ni yale yanayofuata kanuni.

—– Tutaendelea wiki ijayo.

BINTI: UKUAJI – UKOMAVU KATIKA SEHEMU YA UTAMBUZI

Chagua kukataa fedheha ya hedhi kwa mabinti. Amua kudhamini hedhi ya mabinti kutoka familia maskini

Upokeaji na chakataji wa Taarifa

Namna tunavyochakata taarifa tunazozipokea siku hadi siku katika maisha yetu inaathiri aina ya maarifa tunayopkea ndani yetu.  Pia huathiri namna tunavyoweza kuyatumia maarifa hayo yanatokana na taarifa hizo.

Kama ilivyo kwa watu wengine, kwenye hatua ya kuingia katika ubinti na katika hatua za mwanzo za ubinti, binti anaanza kuzichakata taarifa anazopokea. 

Kuanza Kujitambua (Kuongezeka Kimaarifa) Kutokana na Taarifa Anazopokea)

  • Ujuaji unaongezeka au kujithibitisha kimaarifa.  Kwa mfano unaweza kuwa unamweleza jambo yeye anakujibu “najua” kabla hata hujamaliza kuongea. Mtu anaposema “najua” maana yake anathibitisha kwako kiwango chake cha maarifa aliyo nayo katika kulielewa hilo suala unalomwambia.
  • Kuongezeka kwa kiu ya “Maarifa ya Ustadi katika kufanya jambo”: Kwa mfano, anaposema “najua namna ya kufanya …” anaongelea uwezo wake wa kufanya jambo hilo kwa kufuata utaratibu unaotakiwa.  Kwa kiu hii, binti anakuwa kwenye nafasi ya kujifunza maarifa mapya na mbinu mpya kwa urahisi kuliko walipokuwa kwenye hatua waliyokwisha ipita
  • Kuongezeka kwa “Maarifa ya Dhana”:  Haya ni maarifa anayoyapata kwenye kujiuliza maswali kutokana na mambo tofauti anayokutana nayo katika maisha.  Maswali yanayomtaka kujenga dhana ya kile anachokiona au anachosikia.  Uwezo wao mpya wa kufikiri kwa namna ya kutafuta kujua kwanini kitu hicho kipo jinsi kilivyo huwasaidia sio tu kuelewa lakini pia wanaifurahia.
  • Huanza kuziona changamoto katika sura zaidi ya moja:  Katika hatua hii wanaweza kuliona tatizo katika sura tofauti ambazo wakati mwingine baadhi ya hizo sura za tatizo wanazoziona zinaweza kuwa sio muhimu kufanyiwa uamuzi wowote.  Wanakuwa ndio wameingia katika hatua ambayo maisha yanaanza kuwa na changamoto nyingi, hivyo, kuliona kwao tatizo katika sura tofauti huweza kuwapelekea kuchanganyikiwa, kupoteza dira/mwelekeo wa fikra.  Lakini, kwa kadri ambavyo wanajengeka katika kuziona changamoto kwenye sura tofauti wanaimarika zaidi katika kutatua matatizo au changamoto wanazokutana nazo. Ni muhimu sana kuwa karibu nao ili wasije kutatua changamoto katika njia isiyokuwa sahihi.
  • Ubinafsi hujengeka:  Binti katika hatua hii anatumia muda mwingi sana kujifikiria yeye zaidi; anajipa kipaumbele zaidi.  Inaweza kuonekana kama anakuwa mbinafsi kama ukiwa unafikiria kwa akili za kiutu uzima; lakini ni muhimu sana binti kuwa na wakati wa kutafakari juu ya kile anachoamini kwamba ni cha muhimu kwake. Si vizuri kumhukumu bali kumpa ushirikiano hata pale anapokuwa amekusea aelekezwe kwa upendo ambao utamwonyesha alichokosea na apewe elimu ya namna ya kufanya hilo jambo kwa usahihi.  Akipewa ushirikiano sahihi itamsaidia sana kujengeka ndani yake hivyo kuwa rahisi kwake kujitambua na kutambua ni kitu gani anachokitaka katika maisha yake,
  • Tafakari kuhusu Maisha ya Baadaye:  Katika hatua hii ya kukua au kukomaa kwa ufahamu huanza kumjengea binti uwezo wa kutafakari kuhusu maisha yake ya baadaye.  Hii inaanza ule wakati ambao anakuwa yupo na mabinti wenzake, vile vitu ambavyo anakuwa anapenda kuvifanya kulingana vile vitu wanavyoviona au kuvisikia akiwa mbali na wazazi/walezi au ndugu waliowazidi umri.  Anaanza kujilinganisha na hayo mazingira au hivyo vitu na hapo ndipo anapopata nafasi ya kujua ni kipi anakifurahia zaidi na asingependa kuwa mbali nacho katika maisha yake.  Ni kipindi ambacho anaanza kuchagua aina ya maisha anayoyataka na wakati mwingine inaweza kuwa tofauti na kile wazazi/walezi wake wanachofanya.  Huu ni wakati ambao anaanza kutambua na kuainisha malengo ya maisha yake.
  • Hutamani kuelewa uwezo wa kisaikolojia wa watu wengine:  katika kuongeza uwezo wake wa kuchakata taarifa, binti anatamani kuelewa wenzake wanafikiri nini kuhusu jambo fulani ambalo na yeye anakutana nalo.  Anakuwa na tabia ya kuhisi mwenzake anafikiria nini kuhusu hilo jambo kisha anatumia majibu hayo ya kuhisi kujenga uhusiano na mwenzake

Mabinti siku zote hujenga urafiki kwa kulingana na vile wanavyohisi kuhusu saikolojia ya mwenzake na mabinti wengine.  Kwa mfano, binti anayejiona kwamba yeye ni mtanashati, atachagua kuwa rafiki wa binti ambaye ni mtanashati pia.

  • Kubishana kama silaha ya kujenga hoja:  Hii ni namna ya kujijengea uwezo wa kuchambua vitu, anakuwa anataka kujijenga katika kuthibitisha kile anachoamini.
  • Wepesi kufanya maamuzi:  Pamoja na kuwa ni kiwango fulani cha ukomavu katika uwezo wake wa kuchambua vitu, kuna wakati anakuwa mwepesi tu kufanya maamuzi ya kushtukiza.
  • Mara kwa mara ataona kosa anapoonywa au kuelekezwa jambo na mzazi/mlezi wake:  hatua ya ukomavu wake katika kutafakari vitu unampa ujasiri wa kuona mapungufu kutoka kwa mzazi/mlezi.  Anakuwa ana matarajio ya namna ambavyo mzazi/mlezi angemwelekeza kama kuna mahali anakuwa amekosea. Huona kuwa ameonewa.

Binti anahitaji kukua katika na sehemu yake ya utambuzi ili aweze kujitambua hivyo kuwa na afya ya akili hata wanapokuwa watu wazima.  Kuuelewa mchakato wa namna binti anachakata taarifa inakusaidia wewe mzazi/mlezi kujua namna ya kuenenda na binti yako na kumsaidia kisaikolojia kwa kadri anavyokua na kukubiliana na changamoto mbalimbali.

Katika uchakataji wa taarifa binti hupata faida zifuatazo: 

  • Uwezo wa kupambanua vitu huongezeka
  • Uwezo wa kufanya maamuzi sahihi huongezeka
  • Uwezo wa kutunza kumbukumbu na kuzitumia wakati sahihi huimarika
  • Uwezo wa kuchagua aina ya masomo au fani za maisha unaongezeka

….Tutaendelea wiki ijayo kuangalia maeneo mengine ambayo binti hukua kuelekea kwenye umama.

BINTI: UKUAJI

Ukuaji wa mwanadamu ni mchakato endelevu wa maumbile, tabia, ufahamu na hisia.  Kuanzia mwanadamu anapozaliwa kuna hatua mbalimbali anazopitia; uchanga hadi utoto, utoto hadi ujana, ujana hadi utu-uzima na utu-uzima hadi uzee.  Katika hatua zote hizi kuna mabadiliko ya aina tofauti tofauti yanayotokea kulingana na hatua anayokuwepo ama anayoelekea.

Katika kila hatua kila mtu anajijengea mtazamo na tathmini binafsi kuhusu maisha kutokana na vitu vinavyoathiri maisha yake ya kila siku; tathmini binafsi na mtazamo wake humuongoza katika kuwa na aina fulani ya tafsiri kuhusu maisha.  Tafsiri yake kuhusu maisha humsaidia kujijengea imani fulani kuhusu maisha ambapo imani hiyo humpelekea mtu huyo kuwa na kanuni binafsi za maisha.  Hizi kanuni humwongoza katika kufanya maamuzi mbalimbali kwenye mambo yanayohusiana na maisha yake.

Mwanadamu anapotoka kwenye utoto kuingia kwenye ujana, anakua katika nyanja tofauti. Ukuaji katika kila nyanja humjengea mtazamo na tathmini fulani kulingana na watu waliomzunguka na mazingira yaliyomzunguka.

Katika nyanja zote za ukuaji, yaani maumbile, tabia, ufahamu na hisia ni muhimu sana kuwa na taarifa sahihi.  Yaani, ni muhimu kuwa na taarifa kuhusu hiyo hatua ya ukuaji uliyopo na pia kuanza kutaka kujua nini kinakwenda kutokea katika hatua ya ukuaji inayofuatia.

Kama ilivyo muhimu kuwekeza taarifa sahihi kwa mtu kuhusu maendeleo na hatua za ukuaji wa aina mbalimbali kwa mwanadamu, ni muhimu pia kuwekeza taarifa sahihi kuhusu mabadiliko ya ujinsia (sexuality).

Ukuaji wa mtoto wa kike kutoka utoto kwenda ujana, yaani ubinti au msichana, ni tofauti na ukuaji wa mtoto wa kiume kwenda ujana, yaani mvulana.  Hivyo, hata changamoto zao zinatofuatiana sana.  Binti ana changamoto nyingi katika ukuaji wake ukilinganisha na mvulana.

Tutaangalia baadhi ya mabadiliko yanayotokea katika ukuaji wa mtoto wa kike kuelekea ubinti.  Ni muhimu kuwa na taarifa sahihi kwa sababu huu ni wakati ambao vijana wote wa kike na wa kiume wanaanza kujitambua, ni hatua pia ambapo maamuzi mengi ya muhimu kuhusu maisha yao hufanyika.

Yapo mabadiliko ya aina mbalimbali ambayo hutokea katika kipindi hiki.

Kesho tutaanza kuelezea mabadiliko katika kila ukuaji.

Usisahau, tuko kwenye kampeni ya kumsitiri binti ambaye anatoka kwenye familia yenye changamoto ya kiuchumi kiasi cha kushindwa kumnunulia taulo za kike (sanitary pads). Kwa maelezo zaidi ya namna ya kuchangia tafadhali tupigie 0767666048

Mafanikio Yenye Ushawishi

Ukifanikiwa katika kusudi la maisha yako unakuwa maarufu pia kwenye maisha ya watu mbalimbali.  Unapodhamiria kutimiza kusudi la maisha yako ni vyema utambue kwanza umuhimu wa kufanikiwa kwenye maeneo mengine yanayogusa maisha ya watu wengine. 

Hakuna kusudi la maisha la kutimiza pasipo kuona tatizo mahali fulani katika jamii inayokuzunguka. Hivyo ni wajibu wako kuangalia jamii inayokuzunguka na kuangalia ni changamoto ipi kati ya zilizoko katika jamii hiyo ambazo moyo wako unakusukuma kuitatua au kuwa sehemu ya utatuzi.  Mafanikio yanaanza kwa kuitambua changamoto fulani kwenye jamii na kuitatua.

Changamoto ni nyingi kwenye jamii zinazotuzunguka.  Kwa mfano, unaweza kukutana na mtu ambaye anatamani kufanya kile anachotakiwa kufanya lakini hafanyi.  Ni kitu gani unachoweza kumfanyia au kumsaidia mtu kama huyu? Kitu kimoja wapo ni kutumia karama na vipawa ambavyo MUNGU ameweka ndani yako kumsaidia huyu mtu kuziona fursa zinazomzunguka ambazo zinamuwezesha kufanikiwa kwenye kile anachotaka kufanya; lakini pia kumwezesha kuziona changamoto zilizokuwa zinamzuia yeye kufikia lengo lake.  Ukimsaidia kwa njia hii unakuwa umegusa maisha yake kwa namna fulani.

Sio kila wakati tunahitaji kuwa na pesa kuwasaidia watu kutoka kwenye changamoto zao. 

Muhimu:  Jitenge kutoka kwenye kundi la watu wanaoishi maisha ya kawaida, maisha yasiyokuwa na athari yoyote au mguso wowote kwenye jamii inayowazunguka.  Hama kutoka kwenye hayo maisha kwa kutumia kipawa na karama ulizo nazo.  Kuwa mtu mwenye ushawishi kwenye jamii.

Ushawishi ni uwezo wa kuwafanya watu wengine kukusikiliza au kufuatilia kile unachokifanya.  Unakuwa mtu mwenye Ushawishi pale ambapo watu wengine wanabadilisha vipaumbele vyao kwa ajili ya vipaumbele vyako.

Mafanikio yanakufanya uwe mtu mwenye ushawishi katika jamii.  Huwezi kufanikiwa mpaka uwe na ushawishi na huwezi kuwa na ushawishi mpaka umefanikiwa.  Vitu hivi vimeunganika na vinaambatana.

Ni nini asili ya mafanikio?

Tutaendelea wiki ijayo, usikose kutembelea ukurasa huu.

Imeandikwa na:

Lorna Dadi