Nisitiri – DhaminiHedhi Kampeni

Nisitiri – Dhamini Hedhi ni kampeni yenye lengo la kuwafikia mabinti elfu moja kutoka kwenye familia zenye changamoto ya kiuchmi kiasi cha kushindwa kutimiza hitaji la kununuliwa taulo za kike.

Lengo la kampeni hii ni kuwasitiri mabinti hawa wanapokuwa katika hedhi ya mwezi kwa kuwasaidia kupata taulo za kike.  Kama tunavyojua, mwanamke anapokuwa katika hedhi kuna damu inayokuwa inatoka kwenye mwili wake kupitia viungo vyake  za uzazi.  Katika kipindi hiki mwanamke anahitaji kuwa amesitirika ili kwamba ile damu inayotoka kipindi hicho isipitilize na kuonekana kwa nje na mtu mwingine.  Hedhi ni jambo la staha, damu inayotoka inapaswa kuonwa na anayetokwa damu tu na si vinginevyo.  Mwanamke au binti anahitaji taulo za kike kwa ajili ya kujisitiri katika kipindi hiki.

Hedhi ni jambo la asili.  Hedhi ni jambo la uumbaji lililofanywa na MUNGU mwenyewe.  Kila mwanamke aliye kamili huwa na vipindi vya hedhi baada tu ya kuvunja ungo. Hedhi sio jambo ambalo mtu anaweza kuchagua kuwa nayo au kutokuwa nayo.

Inapotokea kwamba, mwanamke au binti yeyote anashindwa kujisitiri katika kipindi hiki cha hedhi, maisha yake hujaa simanzi na unyonge; ujasiri wote humuishia kwani anakuwa katika hali ya mashaka kwamba huenda akachafuka muda wowote kwa damu inayokuwa ikimtoka mwilini mwake kupitia viungo vyake vya uzazi.  Hii damu inapotoka haitoi ishara ya namna yoyote kama vile unapokuwa unasikia haja ndogo au haja kubwa, hii hutoka tu.

Katika mazingira kama haya, binti anapokosa taulo za kike kwa ajili ya kujisitiri kwenye kipindi hiki cha hedhi inamwia vigumu sana kufanya jambo lolote ikiwemo kuhudhuria masomo.

  • Ili mwanafunzi ahudhurie ipasavyo masomo yake anatakiwa ahudhurie siku 194 na vipindi 1740 katika mwaka mmoja wa masomo.
  • Lakini kwa mtoto wa kike hasa wa kijijini amekuwa akikosa masomo kwa wastani wa siku 84 kwa mwaka kutokana na suala la hedhi ambalo ni suala la kimaumbile.
  • Jambo hilo humfanya msichana kukosa kuhudhuria vipindi 756 vyenye Dakika 40 kila kimoja.
  • Hii ni kutokana na changamoto ya kipato cha wazazi wao na pia shule nyingi nchini hasa za vijijini kutokuwa na mazingira rafiki ya usafi kwa wanafunzi wa kike.

Kupitia NISITIRI – Dhamini Hedhi kampeni tunaungana pamoja na serikali, mashirika mbalimbali na jamii kwa ujumla kuhakikisha mtoto wa kike anapata vihifadhi hedhi, yaani taulo za kike, kwa ajili ya kujisitiri katika mzunguko wake wa mwezi lakini pia anapata elimu na uelewa zaidi kuhusu Hedhi salama.

Lengo la kampeni hii ni kuwafikia mabinti elfu moja wanaokaa vijijini. Ni kampeni ya miezi mitano kuanzia 01.02.2020 hadi 30.06.2020. Paketi moja ya taulo za kike itamwezesha binti mmoja kuwa na uhakika wa kuishi bila hofu ya kutokusitirika wakati wa hedhi yake ya mwezi kwa muda wa miaka miwili. Paketi moja inapatikana kwa gharama ya TZS. 10,000/- . Aina ya taulo za kike tunazotegemea kuwapatia ni zile ambazo anaweza kuzifua baada ya kuzitumia. Unaweza kuchangia kupitia https://www.wezeshasasa.com/nisitiri-dhamini-hedhi

Kiwango chochote kuanzia shilingi 1,000/- za Kitanzania.

Asante sana. Karibu ushiriki kwenye kampeni hii yenye mashiko kwa maisha ya binti.