NISITIRI DhaminiHedhi Campaign – Kyela, Mbeya

August, 2020 Nisitiri Reusable Pads ziliwafikia mabinti wa wilaya ya Kyela mkoani Mbeya
Nisitiri Reusable Pads Kyela, Mbeya reach out.

Ilikuwa ni furaha kubwa sana kuweza kuwafikia mabinti hamsini (50) katika wilaya ya Kyela mkoani Mbeya na kuwapatia taulo za kike za Nisitiri.

Mmoja wa mabinti hawa aliileza timu nzima ya Nisitiri Project kwamba taulo hizi ni msaada mkubwa sana kwake kwani kabla ya hapo amekuwa akitumia magodoro yaliyochakaa pindi anapokuwa katika siku zake za hedhi ya mwezi.

Nisitiri Dhamini Hedhi campaign ni kwa ajili ya kuwasaidia mabinti ambao wanatoka katika familia maskini. Familia masikini ambazo hazina uwezo hata wa kukidhi mlo mmoja kwa siku hivyo kufanya suala la kumnunulia binti taulo za kike za kujisitiri wakati wa hedhi kuonekana kama ni anasa.

Campaign hii inahusisha kila mtu mwenye mapenzi mema na mabinti. Hedhi ni fahari ya mwanamke yeyote kwani humpa uhakika kwamba anacho moja kati ya vigezo muhimu sana cha kumpa sifa na uwezo wa kuongeza mwanadamu mwingine duniani.

Nisitiri Reusable Pads zinatayarishwa na LornaDadi Foundation na kutolewa bure kwa wanaufaika, yaani mabinti wenye uhitaji. Gharama za kutayarisha pakti moja ambayo ina taulo nne za kike (sanitary pads) ni kiasi cha TZS. 12,000/- tu. Hatuna mfadhili yoyote rasmi kwa ajili ya project hii bali ni watu mbalimbali (mtu mmoja mmoja) hujitolea kwa kununua hizi pakti kwa kadri wanavyowiwa.

Ikiwa unaguswa na campaign hii tafadhali wasiliana nasi kupitia simu nambari +255 786 666866 au tuma barua pepe kwenda lornadadi@gmail.com

Tunazidi kuwafikia mabinti mbalimbali kutoka sehemu tofauti tofauti za Tanzania. Na siku si nyingi tutaanza kukuletea simulizi za maisha yao ya ubinti hususani changamoto wanazozipitia wakati wa hedhi kupitia youtube channel yetu.

Asante kwa kutembelea website yetu.

MAFANIKIO YENYE USHAWISHI – II

ASILI YA MAFANIKIO

Katika mafanikio kuna vitu viwili ambavyo usipovielewa vinafanyaje kazi katika kuchangia wewe kupata mafanikio yako, utachanganyikiwa.  Vitu hivyo ni Sheria na Kanuni.

Fahamu:  Kuna sehemu ya Kanuni katika mafanikio au kutokufaniniwa kwa mtu binafsi na kuna sehemu ya sheria katika mafanikio au kutokufaniniwa kwa mtu binafsi.

Tofauti ya Sheria na Kanuni

Sheria zinaweza kukuzuia kufikia mafanikio unayotaka kuyafikia.  Yeyote anayetaka kufanikiwa ni lazima avunje sheria za maisha.  Kushindwa kwako katika maisha kunasababishwa na kitendo chako cha kuamua kuwa unatii sheria za maisha.  Usichanganye Sheria na Kanuni.

Kanuni za maisha

Kanuni za maisha hazifanyi kazi kulingana na kile ulichowahi kupitia katika maisha yako au unachopitia sasa, hapana.  Zinafanya kazi wakati wote, haijalishi kama unajua uwepo wa hizo kanuni au hujui.

Mafanikio yanatabirika na kushindwa pia kunatabirika kwa sababu kila kitu katika maisha kiliumbwa kufanya kazi kwa kanuni.  Kanuni huyafanya maisha kutabirika.  Kila kitu kina kanuni inayoambatana nacho kwa sababu kila alichoumba MUNGU kinapaswa kufanikiwa. Kila kitu kinafanikiwa kwa kufuata kanuni.  Kila mtu anafanikiwa kwa kufuata kanuni. 

MUNGU alimuumba mwanadamu kwa ustadi wa kiwango cha hali ya juu sana.  MUNGU aliweka kanuni ambazo endapo mwanadamu atazifuata ni lazima atafanikiwa.  Chochote alichokiumba MUNGU ni lazima kifanikiwe.  Mafanikio ni jambo zuri mbele za MUNGU.

Mafanikio ni muhimu.  Ukitaka kufanikiwa katika maisha usijaribu kufanikiwa katika maisha.  Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu wanajaribu kufanikiwa.  Watu waliofanikiwa hawakujaribu kufaninikiwa, walitekeleza kwa vitendo kanuni za mafanikio na kanuni za maisha.  Kwa maneno mengine, mafanikio ni matokea ya kuwa mtiifu kwenye kanuni.

Mafanikio ni matunda ya shughuli unayojihusisha nayo yaliyotokana na wewe kufuata kanuni.

Unajuaje kama umefanikiwa?

Mafanikio hayapimwi kwa kulinganisha jambo ulilofanya wewe na alilofanya mtu mwingine kwani siku zote wapo watu uliowazidi na waliokuzidi pia.  Mafanikio yanapimwa kwa kulinganisha kati ya kile ulichofanya na kile unachopaswa kufanya.  Mafanikio yanapimwa kupitia nia ya msingi ya wewe kufanya hicho unachofanya.  Mafanikio yako hayapimwi kutokana na kile ulichofanya, hapana, mafanikio yako hupimwa kutokana na lile kusudi la MUNGU kukuumba.  Mafanikio ni utimilifu wa kusudi la MUNGU juu ya maisha yako.  Mafanikio katika maisha yako yanachochewa na kusudi la MUNGU juu ya maisha yako, yaani kile kitu ambacho MUNGU alikuumba uje kukitimiza hapa duniani.  Mafanikio ni kutimia kwa mpango wa MUNGU juu ya maisha yako. Kuna kusudi MUNGU ameweka ndani yako na kuna mahali MUNGU anataka ufike. Haijalishi ni watu wangapi watakusifia, watakushangilia na kukupongeza, kama hukufanya kile kitu ambacho MUNGU anataka ufanye na kama hukufika pale ambapo MUNGU anapotaka ufike, wewe hujafanikiwa. Mafanikio ya Kiungu yanapimwa kwa kufikia ile hatima ambayo MUNGU amekukusudia.  Maisha sio kwa habari ya kufanya kazi kwa bidii lakini kufanya kazi kwa werevu na uhodari kwa kutumia maarifa sahihi.  Utaweza kufanya kazi kwa werevu ukiwa na maarifa yaliyofichwa kwenye kanuni. Chochote unachoanza kufanya au unachoacha kufanya kinategemea zaidi na kanuni unazozifuata au kutozifuata. Kufanikiwa kwako au kushindwa kwako kunategemea na kanuni za maisha unazotii au kutokutii.   Mafanikio sio suala la MUNGU bali ni juu yako wewe mwenyewe.

Mafanikio ni mchakato.  Mafanikio yanavutiwa zaidi na wewe kuwa unaenenda katika mwelekeo sahihi kuliko wewe kufika pale unapokwenda.  Mafanikio ni ule mchakato unaoupitia kuelekea kule unakotakiwa kufika na sio kufika kule unapotakiwa kufika.  Yaani mafanikio yanapatikana hapa njiani kwenye safari ya kuelekea kule unakotaka kufika.  Ukifanikiwa kwa kupitia mchakato sahihi unakuwa umetimiza kusudi lako.

Kama huzijui kanuni za hicho kitu unachotaka kufanikiwa ni dhahiri kwamba hutaweza kuzitii hizo kanuni, Unaposhindwa kuzitii hizo kanuni huwezi kufaninikiwa.  Haijalishi utajibidisha kwa kiwango gani au utamwomba MUNGU kwa kiasi gani.  Mafanikio ni matokea ya kutii kanuni.

Mafanikio yenye ushawishi ni yale yanayofuata kanuni.

—– Tutaendelea wiki ijayo.

BINTI: UKUAJI – UKOMAVU KATIKA SEHEMU YA UTAMBUZI

Chagua kukataa fedheha ya hedhi kwa mabinti. Amua kudhamini hedhi ya mabinti kutoka familia maskini

Upokeaji na chakataji wa Taarifa

Namna tunavyochakata taarifa tunazozipokea siku hadi siku katika maisha yetu inaathiri aina ya maarifa tunayopkea ndani yetu.  Pia huathiri namna tunavyoweza kuyatumia maarifa hayo yanatokana na taarifa hizo.

Kama ilivyo kwa watu wengine, kwenye hatua ya kuingia katika ubinti na katika hatua za mwanzo za ubinti, binti anaanza kuzichakata taarifa anazopokea. 

Kuanza Kujitambua (Kuongezeka Kimaarifa) Kutokana na Taarifa Anazopokea)

  • Ujuaji unaongezeka au kujithibitisha kimaarifa.  Kwa mfano unaweza kuwa unamweleza jambo yeye anakujibu “najua” kabla hata hujamaliza kuongea. Mtu anaposema “najua” maana yake anathibitisha kwako kiwango chake cha maarifa aliyo nayo katika kulielewa hilo suala unalomwambia.
  • Kuongezeka kwa kiu ya “Maarifa ya Ustadi katika kufanya jambo”: Kwa mfano, anaposema “najua namna ya kufanya …” anaongelea uwezo wake wa kufanya jambo hilo kwa kufuata utaratibu unaotakiwa.  Kwa kiu hii, binti anakuwa kwenye nafasi ya kujifunza maarifa mapya na mbinu mpya kwa urahisi kuliko walipokuwa kwenye hatua waliyokwisha ipita
  • Kuongezeka kwa “Maarifa ya Dhana”:  Haya ni maarifa anayoyapata kwenye kujiuliza maswali kutokana na mambo tofauti anayokutana nayo katika maisha.  Maswali yanayomtaka kujenga dhana ya kile anachokiona au anachosikia.  Uwezo wao mpya wa kufikiri kwa namna ya kutafuta kujua kwanini kitu hicho kipo jinsi kilivyo huwasaidia sio tu kuelewa lakini pia wanaifurahia.
  • Huanza kuziona changamoto katika sura zaidi ya moja:  Katika hatua hii wanaweza kuliona tatizo katika sura tofauti ambazo wakati mwingine baadhi ya hizo sura za tatizo wanazoziona zinaweza kuwa sio muhimu kufanyiwa uamuzi wowote.  Wanakuwa ndio wameingia katika hatua ambayo maisha yanaanza kuwa na changamoto nyingi, hivyo, kuliona kwao tatizo katika sura tofauti huweza kuwapelekea kuchanganyikiwa, kupoteza dira/mwelekeo wa fikra.  Lakini, kwa kadri ambavyo wanajengeka katika kuziona changamoto kwenye sura tofauti wanaimarika zaidi katika kutatua matatizo au changamoto wanazokutana nazo. Ni muhimu sana kuwa karibu nao ili wasije kutatua changamoto katika njia isiyokuwa sahihi.
  • Ubinafsi hujengeka:  Binti katika hatua hii anatumia muda mwingi sana kujifikiria yeye zaidi; anajipa kipaumbele zaidi.  Inaweza kuonekana kama anakuwa mbinafsi kama ukiwa unafikiria kwa akili za kiutu uzima; lakini ni muhimu sana binti kuwa na wakati wa kutafakari juu ya kile anachoamini kwamba ni cha muhimu kwake. Si vizuri kumhukumu bali kumpa ushirikiano hata pale anapokuwa amekusea aelekezwe kwa upendo ambao utamwonyesha alichokosea na apewe elimu ya namna ya kufanya hilo jambo kwa usahihi.  Akipewa ushirikiano sahihi itamsaidia sana kujengeka ndani yake hivyo kuwa rahisi kwake kujitambua na kutambua ni kitu gani anachokitaka katika maisha yake,
  • Tafakari kuhusu Maisha ya Baadaye:  Katika hatua hii ya kukua au kukomaa kwa ufahamu huanza kumjengea binti uwezo wa kutafakari kuhusu maisha yake ya baadaye.  Hii inaanza ule wakati ambao anakuwa yupo na mabinti wenzake, vile vitu ambavyo anakuwa anapenda kuvifanya kulingana vile vitu wanavyoviona au kuvisikia akiwa mbali na wazazi/walezi au ndugu waliowazidi umri.  Anaanza kujilinganisha na hayo mazingira au hivyo vitu na hapo ndipo anapopata nafasi ya kujua ni kipi anakifurahia zaidi na asingependa kuwa mbali nacho katika maisha yake.  Ni kipindi ambacho anaanza kuchagua aina ya maisha anayoyataka na wakati mwingine inaweza kuwa tofauti na kile wazazi/walezi wake wanachofanya.  Huu ni wakati ambao anaanza kutambua na kuainisha malengo ya maisha yake.
  • Hutamani kuelewa uwezo wa kisaikolojia wa watu wengine:  katika kuongeza uwezo wake wa kuchakata taarifa, binti anatamani kuelewa wenzake wanafikiri nini kuhusu jambo fulani ambalo na yeye anakutana nalo.  Anakuwa na tabia ya kuhisi mwenzake anafikiria nini kuhusu hilo jambo kisha anatumia majibu hayo ya kuhisi kujenga uhusiano na mwenzake

Mabinti siku zote hujenga urafiki kwa kulingana na vile wanavyohisi kuhusu saikolojia ya mwenzake na mabinti wengine.  Kwa mfano, binti anayejiona kwamba yeye ni mtanashati, atachagua kuwa rafiki wa binti ambaye ni mtanashati pia.

  • Kubishana kama silaha ya kujenga hoja:  Hii ni namna ya kujijengea uwezo wa kuchambua vitu, anakuwa anataka kujijenga katika kuthibitisha kile anachoamini.
  • Wepesi kufanya maamuzi:  Pamoja na kuwa ni kiwango fulani cha ukomavu katika uwezo wake wa kuchambua vitu, kuna wakati anakuwa mwepesi tu kufanya maamuzi ya kushtukiza.
  • Mara kwa mara ataona kosa anapoonywa au kuelekezwa jambo na mzazi/mlezi wake:  hatua ya ukomavu wake katika kutafakari vitu unampa ujasiri wa kuona mapungufu kutoka kwa mzazi/mlezi.  Anakuwa ana matarajio ya namna ambavyo mzazi/mlezi angemwelekeza kama kuna mahali anakuwa amekosea. Huona kuwa ameonewa.

Binti anahitaji kukua katika na sehemu yake ya utambuzi ili aweze kujitambua hivyo kuwa na afya ya akili hata wanapokuwa watu wazima.  Kuuelewa mchakato wa namna binti anachakata taarifa inakusaidia wewe mzazi/mlezi kujua namna ya kuenenda na binti yako na kumsaidia kisaikolojia kwa kadri anavyokua na kukubiliana na changamoto mbalimbali.

Katika uchakataji wa taarifa binti hupata faida zifuatazo: 

  • Uwezo wa kupambanua vitu huongezeka
  • Uwezo wa kufanya maamuzi sahihi huongezeka
  • Uwezo wa kutunza kumbukumbu na kuzitumia wakati sahihi huimarika
  • Uwezo wa kuchagua aina ya masomo au fani za maisha unaongezeka

….Tutaendelea wiki ijayo kuangalia maeneo mengine ambayo binti hukua kuelekea kwenye umama.

BINTI: UKUAJI

Ukuaji wa mwanadamu ni mchakato endelevu wa maumbile, tabia, ufahamu na hisia.  Kuanzia mwanadamu anapozaliwa kuna hatua mbalimbali anazopitia; uchanga hadi utoto, utoto hadi ujana, ujana hadi utu-uzima na utu-uzima hadi uzee.  Katika hatua zote hizi kuna mabadiliko ya aina tofauti tofauti yanayotokea kulingana na hatua anayokuwepo ama anayoelekea.

Katika kila hatua kila mtu anajijengea mtazamo na tathmini binafsi kuhusu maisha kutokana na vitu vinavyoathiri maisha yake ya kila siku; tathmini binafsi na mtazamo wake humuongoza katika kuwa na aina fulani ya tafsiri kuhusu maisha.  Tafsiri yake kuhusu maisha humsaidia kujijengea imani fulani kuhusu maisha ambapo imani hiyo humpelekea mtu huyo kuwa na kanuni binafsi za maisha.  Hizi kanuni humwongoza katika kufanya maamuzi mbalimbali kwenye mambo yanayohusiana na maisha yake.

Mwanadamu anapotoka kwenye utoto kuingia kwenye ujana, anakua katika nyanja tofauti. Ukuaji katika kila nyanja humjengea mtazamo na tathmini fulani kulingana na watu waliomzunguka na mazingira yaliyomzunguka.

Katika nyanja zote za ukuaji, yaani maumbile, tabia, ufahamu na hisia ni muhimu sana kuwa na taarifa sahihi.  Yaani, ni muhimu kuwa na taarifa kuhusu hiyo hatua ya ukuaji uliyopo na pia kuanza kutaka kujua nini kinakwenda kutokea katika hatua ya ukuaji inayofuatia.

Kama ilivyo muhimu kuwekeza taarifa sahihi kwa mtu kuhusu maendeleo na hatua za ukuaji wa aina mbalimbali kwa mwanadamu, ni muhimu pia kuwekeza taarifa sahihi kuhusu mabadiliko ya ujinsia (sexuality).

Ukuaji wa mtoto wa kike kutoka utoto kwenda ujana, yaani ubinti au msichana, ni tofauti na ukuaji wa mtoto wa kiume kwenda ujana, yaani mvulana.  Hivyo, hata changamoto zao zinatofuatiana sana.  Binti ana changamoto nyingi katika ukuaji wake ukilinganisha na mvulana.

Tutaangalia baadhi ya mabadiliko yanayotokea katika ukuaji wa mtoto wa kike kuelekea ubinti.  Ni muhimu kuwa na taarifa sahihi kwa sababu huu ni wakati ambao vijana wote wa kike na wa kiume wanaanza kujitambua, ni hatua pia ambapo maamuzi mengi ya muhimu kuhusu maisha yao hufanyika.

Yapo mabadiliko ya aina mbalimbali ambayo hutokea katika kipindi hiki.

Kesho tutaanza kuelezea mabadiliko katika kila ukuaji.

Usisahau, tuko kwenye kampeni ya kumsitiri binti ambaye anatoka kwenye familia yenye changamoto ya kiuchumi kiasi cha kushindwa kumnunulia taulo za kike (sanitary pads). Kwa maelezo zaidi ya namna ya kuchangia tafadhali tupigie 0767666048

Mafanikio Yenye Ushawishi

Ukifanikiwa katika kusudi la maisha yako unakuwa maarufu pia kwenye maisha ya watu mbalimbali.  Unapodhamiria kutimiza kusudi la maisha yako ni vyema utambue kwanza umuhimu wa kufanikiwa kwenye maeneo mengine yanayogusa maisha ya watu wengine. 

Hakuna kusudi la maisha la kutimiza pasipo kuona tatizo mahali fulani katika jamii inayokuzunguka. Hivyo ni wajibu wako kuangalia jamii inayokuzunguka na kuangalia ni changamoto ipi kati ya zilizoko katika jamii hiyo ambazo moyo wako unakusukuma kuitatua au kuwa sehemu ya utatuzi.  Mafanikio yanaanza kwa kuitambua changamoto fulani kwenye jamii na kuitatua.

Changamoto ni nyingi kwenye jamii zinazotuzunguka.  Kwa mfano, unaweza kukutana na mtu ambaye anatamani kufanya kile anachotakiwa kufanya lakini hafanyi.  Ni kitu gani unachoweza kumfanyia au kumsaidia mtu kama huyu? Kitu kimoja wapo ni kutumia karama na vipawa ambavyo MUNGU ameweka ndani yako kumsaidia huyu mtu kuziona fursa zinazomzunguka ambazo zinamuwezesha kufanikiwa kwenye kile anachotaka kufanya; lakini pia kumwezesha kuziona changamoto zilizokuwa zinamzuia yeye kufikia lengo lake.  Ukimsaidia kwa njia hii unakuwa umegusa maisha yake kwa namna fulani.

Sio kila wakati tunahitaji kuwa na pesa kuwasaidia watu kutoka kwenye changamoto zao. 

Muhimu:  Jitenge kutoka kwenye kundi la watu wanaoishi maisha ya kawaida, maisha yasiyokuwa na athari yoyote au mguso wowote kwenye jamii inayowazunguka.  Hama kutoka kwenye hayo maisha kwa kutumia kipawa na karama ulizo nazo.  Kuwa mtu mwenye ushawishi kwenye jamii.

Ushawishi ni uwezo wa kuwafanya watu wengine kukusikiliza au kufuatilia kile unachokifanya.  Unakuwa mtu mwenye Ushawishi pale ambapo watu wengine wanabadilisha vipaumbele vyao kwa ajili ya vipaumbele vyako.

Mafanikio yanakufanya uwe mtu mwenye ushawishi katika jamii.  Huwezi kufanikiwa mpaka uwe na ushawishi na huwezi kuwa na ushawishi mpaka umefanikiwa.  Vitu hivi vimeunganika na vinaambatana.

Ni nini asili ya mafanikio?

Tutaendelea wiki ijayo, usikose kutembelea ukurasa huu.

Imeandikwa na:

Lorna Dadi