Mafanikio Yenye Ushawishi
Ukifanikiwa katika kusudi la maisha yako unakuwa maarufu pia kwenye maisha ya watu mbalimbali. Unapodhamiria kutimiza kusudi la maisha yako ni vyema utambue kwanza umuhimu wa kufanikiwa kwenye maeneo mengine yanayogusa maisha ya watu wengine.
Hakuna kusudi la maisha la kutimiza pasipo kuona tatizo mahali fulani katika jamii inayokuzunguka. Hivyo ni wajibu wako kuangalia jamii inayokuzunguka na kuangalia ni changamoto ipi kati ya zilizoko katika jamii hiyo ambazo moyo wako unakusukuma kuitatua au kuwa sehemu ya utatuzi. Mafanikio yanaanza kwa kuitambua changamoto fulani kwenye jamii na kuitatua.
Changamoto ni nyingi kwenye jamii zinazotuzunguka. Kwa mfano, unaweza kukutana na mtu ambaye anatamani kufanya kile anachotakiwa kufanya lakini hafanyi. Ni kitu gani unachoweza kumfanyia au kumsaidia mtu kama huyu? Kitu kimoja wapo ni kutumia karama na vipawa ambavyo MUNGU ameweka ndani yako kumsaidia huyu mtu kuziona fursa zinazomzunguka ambazo zinamuwezesha kufanikiwa kwenye kile anachotaka kufanya; lakini pia kumwezesha kuziona changamoto zilizokuwa zinamzuia yeye kufikia lengo lake. Ukimsaidia kwa njia hii unakuwa umegusa maisha yake kwa namna fulani.
Sio kila wakati tunahitaji kuwa na pesa kuwasaidia watu kutoka kwenye changamoto zao.
Muhimu: Jitenge kutoka kwenye kundi la watu wanaoishi maisha ya kawaida, maisha yasiyokuwa na athari yoyote au mguso wowote kwenye jamii inayowazunguka. Hama kutoka kwenye hayo maisha kwa kutumia kipawa na karama ulizo nazo. Kuwa mtu mwenye ushawishi kwenye jamii.
Ushawishi ni uwezo wa kuwafanya watu wengine kukusikiliza au kufuatilia kile unachokifanya. Unakuwa mtu mwenye Ushawishi pale ambapo watu wengine wanabadilisha vipaumbele vyao kwa ajili ya vipaumbele vyako.
Mafanikio yanakufanya uwe mtu mwenye ushawishi katika jamii. Huwezi kufanikiwa mpaka uwe na ushawishi na huwezi kuwa na ushawishi mpaka umefanikiwa. Vitu hivi vimeunganika na vinaambatana.
Ni nini asili ya mafanikio?
Tutaendelea wiki ijayo, usikose kutembelea ukurasa huu.
Imeandikwa na:
Lorna Dadi