BINTI: UKUAJI – UKOMAVU KATIKA SEHEMU YA UTAMBUZI

Chagua kukataa fedheha ya hedhi kwa mabinti. Amua kudhamini hedhi ya mabinti kutoka familia maskini

Upokeaji na chakataji wa Taarifa

Namna tunavyochakata taarifa tunazozipokea siku hadi siku katika maisha yetu inaathiri aina ya maarifa tunayopkea ndani yetu.  Pia huathiri namna tunavyoweza kuyatumia maarifa hayo yanatokana na taarifa hizo.

Kama ilivyo kwa watu wengine, kwenye hatua ya kuingia katika ubinti na katika hatua za mwanzo za ubinti, binti anaanza kuzichakata taarifa anazopokea. 

Kuanza Kujitambua (Kuongezeka Kimaarifa) Kutokana na Taarifa Anazopokea)

 • Ujuaji unaongezeka au kujithibitisha kimaarifa.  Kwa mfano unaweza kuwa unamweleza jambo yeye anakujibu “najua” kabla hata hujamaliza kuongea. Mtu anaposema “najua” maana yake anathibitisha kwako kiwango chake cha maarifa aliyo nayo katika kulielewa hilo suala unalomwambia.
 • Kuongezeka kwa kiu ya “Maarifa ya Ustadi katika kufanya jambo”: Kwa mfano, anaposema “najua namna ya kufanya …” anaongelea uwezo wake wa kufanya jambo hilo kwa kufuata utaratibu unaotakiwa.  Kwa kiu hii, binti anakuwa kwenye nafasi ya kujifunza maarifa mapya na mbinu mpya kwa urahisi kuliko walipokuwa kwenye hatua waliyokwisha ipita
 • Kuongezeka kwa “Maarifa ya Dhana”:  Haya ni maarifa anayoyapata kwenye kujiuliza maswali kutokana na mambo tofauti anayokutana nayo katika maisha.  Maswali yanayomtaka kujenga dhana ya kile anachokiona au anachosikia.  Uwezo wao mpya wa kufikiri kwa namna ya kutafuta kujua kwanini kitu hicho kipo jinsi kilivyo huwasaidia sio tu kuelewa lakini pia wanaifurahia.
 • Huanza kuziona changamoto katika sura zaidi ya moja:  Katika hatua hii wanaweza kuliona tatizo katika sura tofauti ambazo wakati mwingine baadhi ya hizo sura za tatizo wanazoziona zinaweza kuwa sio muhimu kufanyiwa uamuzi wowote.  Wanakuwa ndio wameingia katika hatua ambayo maisha yanaanza kuwa na changamoto nyingi, hivyo, kuliona kwao tatizo katika sura tofauti huweza kuwapelekea kuchanganyikiwa, kupoteza dira/mwelekeo wa fikra.  Lakini, kwa kadri ambavyo wanajengeka katika kuziona changamoto kwenye sura tofauti wanaimarika zaidi katika kutatua matatizo au changamoto wanazokutana nazo. Ni muhimu sana kuwa karibu nao ili wasije kutatua changamoto katika njia isiyokuwa sahihi.
 • Ubinafsi hujengeka:  Binti katika hatua hii anatumia muda mwingi sana kujifikiria yeye zaidi; anajipa kipaumbele zaidi.  Inaweza kuonekana kama anakuwa mbinafsi kama ukiwa unafikiria kwa akili za kiutu uzima; lakini ni muhimu sana binti kuwa na wakati wa kutafakari juu ya kile anachoamini kwamba ni cha muhimu kwake. Si vizuri kumhukumu bali kumpa ushirikiano hata pale anapokuwa amekusea aelekezwe kwa upendo ambao utamwonyesha alichokosea na apewe elimu ya namna ya kufanya hilo jambo kwa usahihi.  Akipewa ushirikiano sahihi itamsaidia sana kujengeka ndani yake hivyo kuwa rahisi kwake kujitambua na kutambua ni kitu gani anachokitaka katika maisha yake,
 • Tafakari kuhusu Maisha ya Baadaye:  Katika hatua hii ya kukua au kukomaa kwa ufahamu huanza kumjengea binti uwezo wa kutafakari kuhusu maisha yake ya baadaye.  Hii inaanza ule wakati ambao anakuwa yupo na mabinti wenzake, vile vitu ambavyo anakuwa anapenda kuvifanya kulingana vile vitu wanavyoviona au kuvisikia akiwa mbali na wazazi/walezi au ndugu waliowazidi umri.  Anaanza kujilinganisha na hayo mazingira au hivyo vitu na hapo ndipo anapopata nafasi ya kujua ni kipi anakifurahia zaidi na asingependa kuwa mbali nacho katika maisha yake.  Ni kipindi ambacho anaanza kuchagua aina ya maisha anayoyataka na wakati mwingine inaweza kuwa tofauti na kile wazazi/walezi wake wanachofanya.  Huu ni wakati ambao anaanza kutambua na kuainisha malengo ya maisha yake.
 • Hutamani kuelewa uwezo wa kisaikolojia wa watu wengine:  katika kuongeza uwezo wake wa kuchakata taarifa, binti anatamani kuelewa wenzake wanafikiri nini kuhusu jambo fulani ambalo na yeye anakutana nalo.  Anakuwa na tabia ya kuhisi mwenzake anafikiria nini kuhusu hilo jambo kisha anatumia majibu hayo ya kuhisi kujenga uhusiano na mwenzake

Mabinti siku zote hujenga urafiki kwa kulingana na vile wanavyohisi kuhusu saikolojia ya mwenzake na mabinti wengine.  Kwa mfano, binti anayejiona kwamba yeye ni mtanashati, atachagua kuwa rafiki wa binti ambaye ni mtanashati pia.

 • Kubishana kama silaha ya kujenga hoja:  Hii ni namna ya kujijengea uwezo wa kuchambua vitu, anakuwa anataka kujijenga katika kuthibitisha kile anachoamini.
 • Wepesi kufanya maamuzi:  Pamoja na kuwa ni kiwango fulani cha ukomavu katika uwezo wake wa kuchambua vitu, kuna wakati anakuwa mwepesi tu kufanya maamuzi ya kushtukiza.
 • Mara kwa mara ataona kosa anapoonywa au kuelekezwa jambo na mzazi/mlezi wake:  hatua ya ukomavu wake katika kutafakari vitu unampa ujasiri wa kuona mapungufu kutoka kwa mzazi/mlezi.  Anakuwa ana matarajio ya namna ambavyo mzazi/mlezi angemwelekeza kama kuna mahali anakuwa amekosea. Huona kuwa ameonewa.

Binti anahitaji kukua katika na sehemu yake ya utambuzi ili aweze kujitambua hivyo kuwa na afya ya akili hata wanapokuwa watu wazima.  Kuuelewa mchakato wa namna binti anachakata taarifa inakusaidia wewe mzazi/mlezi kujua namna ya kuenenda na binti yako na kumsaidia kisaikolojia kwa kadri anavyokua na kukubiliana na changamoto mbalimbali.

Katika uchakataji wa taarifa binti hupata faida zifuatazo: 

 • Uwezo wa kupambanua vitu huongezeka
 • Uwezo wa kufanya maamuzi sahihi huongezeka
 • Uwezo wa kutunza kumbukumbu na kuzitumia wakati sahihi huimarika
 • Uwezo wa kuchagua aina ya masomo au fani za maisha unaongezeka

….Tutaendelea wiki ijayo kuangalia maeneo mengine ambayo binti hukua kuelekea kwenye umama.

BINTI: UKUAJI

Ukuaji wa mwanadamu ni mchakato endelevu wa maumbile, tabia, ufahamu na hisia.  Kuanzia mwanadamu anapozaliwa kuna hatua mbalimbali anazopitia; uchanga hadi utoto, utoto hadi ujana, ujana hadi utu-uzima na utu-uzima hadi uzee.  Katika hatua zote hizi kuna mabadiliko ya aina tofauti tofauti yanayotokea kulingana na hatua anayokuwepo ama anayoelekea.

Katika kila hatua kila mtu anajijengea mtazamo na tathmini binafsi kuhusu maisha kutokana na vitu vinavyoathiri maisha yake ya kila siku; tathmini binafsi na mtazamo wake humuongoza katika kuwa na aina fulani ya tafsiri kuhusu maisha.  Tafsiri yake kuhusu maisha humsaidia kujijengea imani fulani kuhusu maisha ambapo imani hiyo humpelekea mtu huyo kuwa na kanuni binafsi za maisha.  Hizi kanuni humwongoza katika kufanya maamuzi mbalimbali kwenye mambo yanayohusiana na maisha yake.

Mwanadamu anapotoka kwenye utoto kuingia kwenye ujana, anakua katika nyanja tofauti. Ukuaji katika kila nyanja humjengea mtazamo na tathmini fulani kulingana na watu waliomzunguka na mazingira yaliyomzunguka.

Katika nyanja zote za ukuaji, yaani maumbile, tabia, ufahamu na hisia ni muhimu sana kuwa na taarifa sahihi.  Yaani, ni muhimu kuwa na taarifa kuhusu hiyo hatua ya ukuaji uliyopo na pia kuanza kutaka kujua nini kinakwenda kutokea katika hatua ya ukuaji inayofuatia.

Kama ilivyo muhimu kuwekeza taarifa sahihi kwa mtu kuhusu maendeleo na hatua za ukuaji wa aina mbalimbali kwa mwanadamu, ni muhimu pia kuwekeza taarifa sahihi kuhusu mabadiliko ya ujinsia (sexuality).

Ukuaji wa mtoto wa kike kutoka utoto kwenda ujana, yaani ubinti au msichana, ni tofauti na ukuaji wa mtoto wa kiume kwenda ujana, yaani mvulana.  Hivyo, hata changamoto zao zinatofuatiana sana.  Binti ana changamoto nyingi katika ukuaji wake ukilinganisha na mvulana.

Tutaangalia baadhi ya mabadiliko yanayotokea katika ukuaji wa mtoto wa kike kuelekea ubinti.  Ni muhimu kuwa na taarifa sahihi kwa sababu huu ni wakati ambao vijana wote wa kike na wa kiume wanaanza kujitambua, ni hatua pia ambapo maamuzi mengi ya muhimu kuhusu maisha yao hufanyika.

Yapo mabadiliko ya aina mbalimbali ambayo hutokea katika kipindi hiki.

Kesho tutaanza kuelezea mabadiliko katika kila ukuaji.

Usisahau, tuko kwenye kampeni ya kumsitiri binti ambaye anatoka kwenye familia yenye changamoto ya kiuchumi kiasi cha kushindwa kumnunulia taulo za kike (sanitary pads). Kwa maelezo zaidi ya namna ya kuchangia tafadhali tupigie 0767666048