KUWA MWENYE FURAHA
Ni vizuri kuwa mwenye furaha! Je, unajua kuwa kuna njia nyingi unazoweza kujisaidia wewe mwenyewe kuwa mwenye furaha?
Hizi ni baadhi ya zile ambazo mimi huwa natumia kujisaidia kuwa mwenye furaha:
- Najitahidi kuimarisha uhusiano wangu na MUNGU nyakati zote: za vicheko ama vilio, raha ama huzuni, kukosa ama kupata, kupanda ama kushuka, nk.
- Kushughulisha akili yangu zaidi kwa mambo yanayoleta mtazamo chanya wa maisha
- Hupenda kuufanyisha mwili wako mazoezi, (nafanya mazoezi madogo madogo sana kwa wafanya mazoezi hawawezi kuyaita ya kwangu ni mazoezi). Kufanya mazoezi huchangia sana kuwa na afya bora sio tu ya mwili bali na akili pia.
- Najitahidi kulala usingizi wenye utulivu. kwa watu wanaonijua wanasemaga “Lorna ana kifurushi cha kutosha cha usingizi”. Hii ni kwa sababu, linapokuja suala la kulala hata kama ni nusu saa tu mimi kwa kweli huwa nahakikisha nimelala. Na ninapolala akili yangu, moyo wangu, roho yangu na mwili wangu najitahidi sana viwe katika utulivu. Kuchoka sana kunaweza kuharibu hisia zako. Watu ambao hawana usingizi wa kutosha au hawapati usingizi tulivu wataalamu wanasema wapo kwenye hatari kubwa sana ya kupata tatizo la msongo wa mawazo.
- Najitahidi kupata mlo sahihi kwa wakati sahihi. Mwili usipopata nguvu ya kutosha kwa kadri inavyohitajika kuna vitu havitaenda sawa katika mfumo mzima wa utendaji kazi wa mwili; hii huathiri hata uwezo au utendaji kazi wa akili ya mtu pia.
- Najitahidi kujenga mahusiano mazuri na watu tofauti kwa kadri ninavyokutana nao katika nyanja na hatua mbalimbali za maisha yangu. Naamini kwamba kuwa na mahusiano sahihi kunatengenezwa zaidi na kuwa na mawasiliano sahihi. Ninajitahidi kumweka kila mtu ninayekutana naye kwenye maisha yangu kwenye nafasi anayostahili kuwekwa na mimi ndani nyangu. Huwa nina akiba ya namna ninavyomchukulia mtu. Hii inanisaidia kujiepusha na vitu kama vile kumtarajia mtu awe wa aina fulani kwangu kumbe yeye kwangu mimi alivyojiweka ni tofauti na ninavyomchukulia.
- Ninalinda sana kile kilicho ndani yangu. Huwa siruhusu mtu yeyote aniburuze kwa namna yoyote ile; iwe hisia zangu, werevu wangu, nguvu zangu, maono yangu, moyo wangu au kitu kingine chochote kile ambacho kiuhalisia ni cha kwangu ambacho MUNGU ameweka ndani yangu. Huku Duniani kuna watu wanajua jinsi ya kurudisha watu wengine nyuma; anaweza kukufanya ukajihisi mjinga, huwezi kabisa kufanya chochote au ndoto uliyo nayo ni ujinga tu! Watu wa aina hii ukiwapa nafasi kwenye maisha yako ni rahisi sana kukubadilisha namna unavyofikiria kuhusu wewe mwenyewe. Unavyojifikiria kuhusu wewe mwenyewe ni nguzu muhimu sana ya maisha yako na kile kinachokwenda kudhihirika kwenye maisha yako. Ninaamini kwamba jinsi ninavyojisikia kujihusu na jinsi ninavyoamini kuhusu mimi mwenyewe huathiri sana mtazamo na imani yangu jinsi ninavyoamini kuhusu maisha na ninavyoyachukulia maisha kwa ujumla
- Ninatambua kwamba haijalishi nitafanya kitu chenye fedha nyingi kiasi gani au kunitanisha na watu maarufu kiasi gani au mimi mwenyewe kuwa maarufu kiasi gani, kama sitaishi maisha aliyonikusudia MUNGU kuishi hapa Duniani basi kamwe siwezi kuwa na furaha ya kweli maishani mwangu. Ninaamini kwamba, maisha yanayoweza kuni furaha ya kamili ni maisha ya kuziidhi ndoto zangu, maisha ya kuliishi kusudi la maisha yangu na maono MUNGU aliyoweka ndani yangu. Na nimechagua kukubali kwamba, jukumu la kutimiza maono yangu au ndoto zangu ni la kwangu mwenyewe.
- Siruhusu mtu yeyote yule au kitu chochote kile asimame au kisimame kama kikwazo cha mimi kutekeleza ninachopaswa kutekeleza ili kutimiza maono yangu. Na wala sihamishi jukumu la utekelezaji wa maono yangu au ndoto zangu kwa mtu mwingine yeyote yule.
- Ninaamini kwamba watu ambao MUNGU amewakusudia kuwa na mimi katika kutekeleza maono aliyoweka ndani yangu kwenye hatua tofauti tofauti za maono hayo, sio kila mtu ni sehemu ya ndoto au maono yangu haijalishi ni mtu wa karibu kwangu kiasi gani. Hii inanisaidi kuimarisha uhusiano wangu na watu wasionisapoti kwenye maono yangu.
- Naamini katika kusaidia weninge pale ninapoweza kufanya hivyo. Kusaidia watu wengine kunanipatia hisia za kusihi maisha yenye mguso kwa weninge hivyo kuniondolea kiburi cha kujiona mimi ni bora zaidi au ninastahili zaidi vitu fulani vya maisha kuliko kwengine. Ninaamini kwenye kutenda mema hapa Duniani.
- Najitahidi kuwa mwaminifu kwangu mwenyewe. Kwa kufanya hivi ninaweza kutimiza vitu vingi ambavyo nimejiwekea malengo mwenyewe. Nisipokuwa mwaminifu juu yangu au juu ya mambo yangu mwenyewe kamwe siwezi kuwa mwaminifu kwa watu wengine au mambo yanayohusu watu wengine.
Je ipo yoyote unayoona inakufaa katika ya hizo kumi na mbili?
Je, wewe unatumia njia gani au unafanya vitu gani kuhakikisha una furaha muda mwingi?
Niandikie hapo chini kwenye comment ili mimi na wengine tujifunze zaidi na kuboresha maisha yetu ya ndani. Furaha ya kweli huboresha maisha yetu ya ndani. Maisha yetu ya nje ni tafsiri ya maisha yetu ya ndani.