BINTI: UKUAJI

Ukuaji wa mwanadamu ni mchakato endelevu wa maumbile, tabia, ufahamu na hisia.  Kuanzia mwanadamu anapozaliwa kuna hatua mbalimbali anazopitia; uchanga hadi utoto, utoto hadi ujana, ujana hadi utu-uzima na utu-uzima hadi uzee.  Katika hatua zote hizi kuna mabadiliko ya aina tofauti tofauti yanayotokea kulingana na hatua anayokuwepo ama anayoelekea.

Katika kila hatua kila mtu anajijengea mtazamo na tathmini binafsi kuhusu maisha kutokana na vitu vinavyoathiri maisha yake ya kila siku; tathmini binafsi na mtazamo wake humuongoza katika kuwa na aina fulani ya tafsiri kuhusu maisha.  Tafsiri yake kuhusu maisha humsaidia kujijengea imani fulani kuhusu maisha ambapo imani hiyo humpelekea mtu huyo kuwa na kanuni binafsi za maisha.  Hizi kanuni humwongoza katika kufanya maamuzi mbalimbali kwenye mambo yanayohusiana na maisha yake.

Mwanadamu anapotoka kwenye utoto kuingia kwenye ujana, anakua katika nyanja tofauti. Ukuaji katika kila nyanja humjengea mtazamo na tathmini fulani kulingana na watu waliomzunguka na mazingira yaliyomzunguka.

Katika nyanja zote za ukuaji, yaani maumbile, tabia, ufahamu na hisia ni muhimu sana kuwa na taarifa sahihi.  Yaani, ni muhimu kuwa na taarifa kuhusu hiyo hatua ya ukuaji uliyopo na pia kuanza kutaka kujua nini kinakwenda kutokea katika hatua ya ukuaji inayofuatia.

Kama ilivyo muhimu kuwekeza taarifa sahihi kwa mtu kuhusu maendeleo na hatua za ukuaji wa aina mbalimbali kwa mwanadamu, ni muhimu pia kuwekeza taarifa sahihi kuhusu mabadiliko ya ujinsia (sexuality).

Ukuaji wa mtoto wa kike kutoka utoto kwenda ujana, yaani ubinti au msichana, ni tofauti na ukuaji wa mtoto wa kiume kwenda ujana, yaani mvulana.  Hivyo, hata changamoto zao zinatofuatiana sana.  Binti ana changamoto nyingi katika ukuaji wake ukilinganisha na mvulana.

Tutaangalia baadhi ya mabadiliko yanayotokea katika ukuaji wa mtoto wa kike kuelekea ubinti.  Ni muhimu kuwa na taarifa sahihi kwa sababu huu ni wakati ambao vijana wote wa kike na wa kiume wanaanza kujitambua, ni hatua pia ambapo maamuzi mengi ya muhimu kuhusu maisha yao hufanyika.

Yapo mabadiliko ya aina mbalimbali ambayo hutokea katika kipindi hiki.

Kesho tutaanza kuelezea mabadiliko katika kila ukuaji.

Usisahau, tuko kwenye kampeni ya kumsitiri binti ambaye anatoka kwenye familia yenye changamoto ya kiuchumi kiasi cha kushindwa kumnunulia taulo za kike (sanitary pads). Kwa maelezo zaidi ya namna ya kuchangia tafadhali tupigie 0767666048