Ilikuwa ni furaha kubwa sana kuweza kuwafikia mabinti hamsini (50) katika wilaya ya Kyela mkoani Mbeya na kuwapatia taulo za kike za Nisitiri.
Mmoja wa mabinti hawa aliileza timu nzima ya Nisitiri Project kwamba taulo hizi ni msaada mkubwa sana kwake kwani kabla ya hapo amekuwa akitumia magodoro yaliyochakaa pindi anapokuwa katika siku zake za hedhi ya mwezi.
Nisitiri Dhamini Hedhi campaign ni kwa ajili ya kuwasaidia mabinti ambao wanatoka katika familia maskini. Familia masikini ambazo hazina uwezo hata wa kukidhi mlo mmoja kwa siku hivyo kufanya suala la kumnunulia binti taulo za kike za kujisitiri wakati wa hedhi kuonekana kama ni anasa.
Campaign hii inahusisha kila mtu mwenye mapenzi mema na mabinti. Hedhi ni fahari ya mwanamke yeyote kwani humpa uhakika kwamba anacho moja kati ya vigezo muhimu sana cha kumpa sifa na uwezo wa kuongeza mwanadamu mwingine duniani.
Nisitiri Reusable Pads zinatayarishwa na LornaDadi Foundation na kutolewa bure kwa wanaufaika, yaani mabinti wenye uhitaji. Gharama za kutayarisha pakti moja ambayo ina taulo nne za kike (sanitary pads) ni kiasi cha TZS. 12,000/- tu. Hatuna mfadhili yoyote rasmi kwa ajili ya project hii bali ni watu mbalimbali (mtu mmoja mmoja) hujitolea kwa kununua hizi pakti kwa kadri wanavyowiwa.
Ikiwa unaguswa na campaign hii tafadhali wasiliana nasi kupitia simu nambari +255 786 666866 au tuma barua pepe kwenda lornadadi@gmail.com
Tunazidi kuwafikia mabinti mbalimbali kutoka sehemu tofauti tofauti za Tanzania. Na siku si nyingi tutaanza kukuletea simulizi za maisha yao ya ubinti hususani changamoto wanazozipitia wakati wa hedhi kupitia youtube channel yetu.
Katika mafanikio kuna vitu
viwili ambavyo usipovielewa vinafanyaje kazi katika kuchangia wewe kupata
mafanikio yako, utachanganyikiwa. Vitu
hivyo ni Sheria na Kanuni.
Fahamu: Kuna sehemu ya Kanuni katika mafanikio au
kutokufaniniwa kwa mtu binafsi na kuna sehemu ya sheria katika mafanikio au
kutokufaniniwa kwa mtu binafsi.
Tofauti ya Sheria na
Kanuni
Sheria zinaweza kukuzuia kufikia mafanikio unayotaka kuyafikia. Yeyote anayetaka kufanikiwa ni lazima avunje sheria za maisha. Kushindwa kwako katika maisha kunasababishwa na kitendo chako cha kuamua kuwa unatii sheria za maisha. Usichanganye Sheria na Kanuni.
Kanuni za maisha
Kanuni za maisha hazifanyi kazi
kulingana na kile ulichowahi kupitia katika maisha yako au unachopitia sasa,
hapana. Zinafanya kazi wakati wote, haijalishi
kama unajua uwepo wa hizo kanuni au hujui.
Mafanikio yanatabirika na kushindwa
pia kunatabirika kwa sababu kila kitu katika maisha kiliumbwa kufanya kazi kwa
kanuni. Kanuni huyafanya maisha
kutabirika. Kila kitu kina kanuni inayoambatana
nacho kwa sababu kila alichoumba MUNGU kinapaswa kufanikiwa. Kila kitu
kinafanikiwa kwa kufuata kanuni. Kila
mtu anafanikiwa kwa kufuata kanuni.
MUNGU alimuumba mwanadamu kwa ustadi wa kiwango cha hali ya juu sana. MUNGU aliweka kanuni ambazo endapo mwanadamu atazifuata ni lazima atafanikiwa. Chochote alichokiumba MUNGU ni lazima kifanikiwe. Mafanikio ni jambo zuri mbele za MUNGU.
Mafanikio ni muhimu. Ukitaka kufanikiwa katika maisha usijaribu kufanikiwa katika maisha. Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa sababu wanajaribu kufanikiwa. Watu waliofanikiwa hawakujaribu kufaninikiwa, walitekeleza kwa vitendo kanuni za mafanikio na kanuni za maisha. Kwa maneno mengine, mafanikio ni matokea ya kuwa mtiifu kwenye kanuni.
Mafanikio ni matunda ya shughuli unayojihusisha nayo yaliyotokana na wewe kufuata kanuni.
Unajuaje kama
umefanikiwa?
Mafanikio hayapimwi kwa kulinganisha jambo ulilofanya wewe na alilofanya mtu mwingine kwani siku zote wapo watu uliowazidi na waliokuzidi pia. Mafanikio yanapimwa kwa kulinganisha kati ya kile ulichofanya na kile unachopaswa kufanya. Mafanikio yanapimwa kupitia nia ya msingi ya wewe kufanya hicho unachofanya. Mafanikio yako hayapimwi kutokana na kile ulichofanya, hapana, mafanikio yako hupimwa kutokana na lile kusudi la MUNGU kukuumba. Mafanikio ni utimilifu wa kusudi la MUNGU juu ya maisha yako. Mafanikio katika maisha yako yanachochewa na kusudi la MUNGU juu ya maisha yako, yaani kile kitu ambacho MUNGU alikuumba uje kukitimiza hapa duniani. Mafanikio ni kutimia kwa mpango wa MUNGU juu ya maisha yako. Kuna kusudi MUNGU ameweka ndani yako na kuna mahali MUNGU anataka ufike. Haijalishi ni watu wangapi watakusifia, watakushangilia na kukupongeza, kama hukufanya kile kitu ambacho MUNGU anataka ufanye na kama hukufika pale ambapo MUNGU anapotaka ufike, wewe hujafanikiwa. Mafanikio ya Kiungu yanapimwa kwa kufikia ile hatima ambayo MUNGU amekukusudia. Maisha sio kwa habari ya kufanya kazi kwa bidii lakini kufanya kazi kwa werevu na uhodari kwa kutumia maarifa sahihi. Utaweza kufanya kazi kwa werevu ukiwa na maarifa yaliyofichwa kwenye kanuni. Chochote unachoanza kufanya au unachoacha kufanya kinategemea zaidi na kanuni unazozifuata au kutozifuata. Kufanikiwa kwako au kushindwa kwako kunategemea na kanuni za maisha unazotii au kutokutii. Mafanikio sio suala la MUNGU bali ni juu yako wewe mwenyewe.
Mafanikio ni mchakato. Mafanikio yanavutiwa zaidi na wewe kuwa unaenenda katika mwelekeo sahihi kuliko wewe kufika pale unapokwenda. Mafanikio ni ule mchakato unaoupitia kuelekea kule unakotakiwa kufika na sio kufika kule unapotakiwa kufika. Yaani mafanikio yanapatikana hapa njiani kwenye safari ya kuelekea kule unakotaka kufika. Ukifanikiwa kwa kupitia mchakato sahihi unakuwa umetimiza kusudi lako.
Kama huzijui kanuni za hicho kitu unachotaka kufanikiwa ni dhahiri kwamba hutaweza kuzitii hizo kanuni, Unaposhindwa kuzitii hizo kanuni huwezi kufaninikiwa. Haijalishi utajibidisha kwa kiwango gani au utamwomba MUNGU kwa kiasi gani. Mafanikio ni matokea ya kutii kanuni.
Mafanikio
yenye ushawishi ni yale yanayofuata kanuni.
—– Tutaendelea wiki ijayo.
http://lornadadi.com/wp-content/uploads/2017/02/ldf-logo.png00lornadfhttp://lornadadi.com/wp-content/uploads/2017/02/ldf-logo.pnglornadf2020-02-19 11:31:082020-02-19 11:46:22MAFANIKIO YENYE USHAWISHI – II
Namna tunavyochakata taarifa
tunazozipokea siku hadi siku katika maisha yetu inaathiri aina ya maarifa tunayopkea
ndani yetu. Pia huathiri namna tunavyoweza
kuyatumia maarifa hayo yanatokana na taarifa hizo.
Kama ilivyo kwa watu wengine, kwenye
hatua ya kuingia katika ubinti na katika hatua za mwanzo za ubinti, binti
anaanza kuzichakata taarifa anazopokea.
Kuanza Kujitambua
(Kuongezeka Kimaarifa) Kutokana na Taarifa Anazopokea)
Ujuaji unaongezeka au kujithibitisha kimaarifa. Kwa mfano unaweza kuwa unamweleza jambo yeye
anakujibu “najua” kabla hata hujamaliza kuongea. Mtu anaposema “najua” maana
yake anathibitisha kwako kiwango chake cha maarifa aliyo nayo katika kulielewa
hilo suala unalomwambia.
Kuongezeka kwa kiu ya “Maarifa ya Ustadi katika kufanya
jambo”: Kwa mfano, anaposema
“najua namna ya kufanya …” anaongelea uwezo wake wa kufanya jambo hilo kwa
kufuata utaratibu unaotakiwa. Kwa kiu
hii, binti anakuwa kwenye nafasi ya kujifunza maarifa mapya na mbinu mpya kwa
urahisi kuliko walipokuwa kwenye hatua waliyokwisha ipita
Kuongezeka kwa “Maarifa
ya Dhana”: Haya ni
maarifa anayoyapata kwenye kujiuliza maswali kutokana na mambo tofauti
anayokutana nayo katika maisha. Maswali
yanayomtaka kujenga dhana ya kile anachokiona au anachosikia. Uwezo wao mpya wa kufikiri kwa namna ya
kutafuta kujua kwanini kitu hicho kipo jinsi kilivyo huwasaidia sio tu kuelewa
lakini pia wanaifurahia.
Huanza kuziona changamoto katika sura zaidi ya moja: Katika hatua hii wanaweza kuliona tatizo
katika sura tofauti ambazo wakati mwingine baadhi ya hizo sura za tatizo
wanazoziona zinaweza kuwa sio muhimu kufanyiwa uamuzi wowote. Wanakuwa ndio wameingia katika hatua ambayo
maisha yanaanza kuwa na changamoto nyingi, hivyo, kuliona kwao tatizo katika
sura tofauti huweza kuwapelekea kuchanganyikiwa, kupoteza dira/mwelekeo wa
fikra. Lakini, kwa kadri ambavyo
wanajengeka katika kuziona changamoto kwenye sura tofauti wanaimarika zaidi
katika kutatua matatizo au changamoto wanazokutana nazo. Ni muhimu sana kuwa
karibu nao ili wasije kutatua changamoto katika njia isiyokuwa sahihi.
Ubinafsi
hujengeka: Binti katika hatua hii anatumia muda mwingi
sana kujifikiria yeye zaidi; anajipa kipaumbele zaidi. Inaweza kuonekana kama anakuwa mbinafsi kama
ukiwa unafikiria kwa akili za kiutu uzima; lakini ni muhimu sana binti kuwa na
wakati wa kutafakari juu ya kile anachoamini kwamba ni cha muhimu kwake. Si
vizuri kumhukumu bali kumpa ushirikiano hata pale anapokuwa amekusea aelekezwe
kwa upendo ambao utamwonyesha alichokosea na apewe elimu ya namna ya kufanya
hilo jambo kwa usahihi. Akipewa
ushirikiano sahihi itamsaidia sana kujengeka ndani yake hivyo kuwa rahisi kwake
kujitambua na kutambua ni kitu gani anachokitaka katika maisha yake,
Tafakari kuhusu Maisha ya Baadaye: Katika hatua hii ya kukua au kukomaa kwa ufahamu
huanza kumjengea binti uwezo wa kutafakari kuhusu maisha yake ya baadaye. Hii inaanza ule wakati ambao anakuwa yupo na mabinti
wenzake, vile vitu ambavyo anakuwa anapenda kuvifanya kulingana vile vitu
wanavyoviona au kuvisikia akiwa mbali na wazazi/walezi au ndugu waliowazidi
umri. Anaanza kujilinganisha na hayo
mazingira au hivyo vitu na hapo ndipo anapopata nafasi ya kujua ni kipi
anakifurahia zaidi na asingependa kuwa mbali nacho katika maisha yake. Ni kipindi ambacho anaanza kuchagua aina ya
maisha anayoyataka na wakati mwingine inaweza kuwa tofauti na kile
wazazi/walezi wake wanachofanya. Huu ni
wakati ambao anaanza kutambua na kuainisha malengo ya maisha yake.
Hutamani kuelewa uwezo wa kisaikolojia wa watu
wengine:katika kuongeza uwezo wake wa kuchakata
taarifa, binti anatamani kuelewa wenzake wanafikiri nini kuhusu jambo fulani
ambalo na yeye anakutana nalo. Anakuwa na
tabia ya kuhisi mwenzake anafikiria nini kuhusu hilo jambo kisha anatumia
majibu hayo ya kuhisi kujenga uhusiano na mwenzake
Mabinti siku
zote hujenga urafiki kwa kulingana na vile wanavyohisi kuhusu saikolojia ya
mwenzake na mabinti wengine. Kwa mfano,
binti anayejiona kwamba yeye ni mtanashati, atachagua kuwa rafiki wa binti
ambaye ni mtanashati pia.
Kubishana kama silaha ya kujenga hoja: Hii ni namna ya kujijengea uwezo wa kuchambua
vitu, anakuwa anataka kujijenga katika kuthibitisha kile anachoamini.
Wepesi kufanya maamuzi: Pamoja na kuwa ni kiwango fulani cha ukomavu
katika uwezo wake wa kuchambua vitu, kuna wakati anakuwa mwepesi tu kufanya
maamuzi ya kushtukiza.
Mara kwa mara ataona kosa anapoonywa au kuelekezwa
jambo na mzazi/mlezi wake: hatua
ya ukomavu wake katika kutafakari vitu unampa ujasiri wa kuona mapungufu kutoka
kwa mzazi/mlezi. Anakuwa ana matarajio
ya namna ambavyo mzazi/mlezi angemwelekeza kama kuna mahali anakuwa amekosea.
Huona kuwa ameonewa.
Binti anahitaji kukua katika na sehemu
yake ya utambuzi ili aweze kujitambua hivyo kuwa na afya ya akili hata
wanapokuwa watu wazima. Kuuelewa
mchakato wa namna binti anachakata taarifa inakusaidia wewe mzazi/mlezi kujua
namna ya kuenenda na binti yako na kumsaidia kisaikolojia kwa kadri anavyokua
na kukubiliana na changamoto mbalimbali.
Katika
uchakataji wa taarifa binti hupata faida zifuatazo:
Uwezo wa kupambanua vitu huongezeka
Uwezo wa kufanya maamuzi sahihi huongezeka
Uwezo wa kutunza kumbukumbu na kuzitumia wakati
sahihi huimarika
Uwezo wa kuchagua aina ya masomo au fani za maisha
unaongezeka
….Tutaendelea wiki ijayo kuangalia maeneo mengine ambayo binti hukua kuelekea kwenye umama.
http://lornadadi.com/wp-content/uploads/2017/02/ldf-logo.png00lornadfhttp://lornadadi.com/wp-content/uploads/2017/02/ldf-logo.pnglornadf2020-02-18 20:05:552020-02-18 20:06:00BINTI: UKUAJI – UKOMAVU KATIKA SEHEMU YA UTAMBUZI
Ukuaji wa mwanadamu ni
mchakato endelevu wa maumbile, tabia, ufahamu na hisia. Kuanzia mwanadamu anapozaliwa kuna hatua
mbalimbali anazopitia; uchanga hadi utoto, utoto hadi ujana, ujana hadi utu-uzima
na utu-uzima hadi uzee. Katika hatua
zote hizi kuna mabadiliko ya aina tofauti tofauti yanayotokea kulingana na
hatua anayokuwepo ama anayoelekea.
Katika kila hatua kila mtu
anajijengea mtazamo na tathmini binafsi kuhusu maisha kutokana na vitu vinavyoathiri
maisha yake ya kila siku; tathmini binafsi na mtazamo wake humuongoza katika kuwa
na aina fulani ya tafsiri kuhusu maisha.
Tafsiri yake kuhusu maisha humsaidia kujijengea imani fulani kuhusu
maisha ambapo imani hiyo humpelekea mtu huyo kuwa na kanuni binafsi za maisha. Hizi kanuni humwongoza katika kufanya maamuzi
mbalimbali kwenye mambo yanayohusiana na maisha yake.
Mwanadamu anapotoka kwenye
utoto kuingia kwenye ujana, anakua katika nyanja tofauti. Ukuaji katika kila
nyanja humjengea mtazamo na tathmini fulani kulingana na watu waliomzunguka na
mazingira yaliyomzunguka.
Katika nyanja zote za ukuaji,
yaani maumbile, tabia, ufahamu na hisia ni muhimu sana kuwa na taarifa
sahihi. Yaani, ni muhimu kuwa na taarifa
kuhusu hiyo hatua ya ukuaji uliyopo na pia kuanza kutaka kujua nini kinakwenda
kutokea katika hatua ya ukuaji inayofuatia.
Kama ilivyo muhimu kuwekeza
taarifa sahihi kwa mtu kuhusu maendeleo na hatua za ukuaji wa aina mbalimbali kwa
mwanadamu, ni muhimu pia kuwekeza taarifa sahihi kuhusu mabadiliko ya ujinsia
(sexuality).
Ukuaji wa mtoto wa kike kutoka
utoto kwenda ujana, yaani ubinti au msichana, ni tofauti na ukuaji wa mtoto wa
kiume kwenda ujana, yaani mvulana. Hivyo,
hata changamoto zao zinatofuatiana sana.
Binti ana changamoto nyingi katika ukuaji wake ukilinganisha na mvulana.
Tutaangalia baadhi ya mabadiliko
yanayotokea katika ukuaji wa mtoto wa kike kuelekea ubinti. Ni muhimu kuwa na taarifa sahihi kwa sababu
huu ni wakati ambao vijana wote wa kike na wa kiume wanaanza kujitambua, ni hatua
pia ambapo maamuzi mengi ya muhimu kuhusu maisha yao hufanyika.
Yapo mabadiliko ya aina
mbalimbali ambayo hutokea katika kipindi hiki.
Kesho tutaanza kuelezea mabadiliko katika kila ukuaji.
Usisahau, tuko kwenye kampeni ya kumsitiri binti ambaye anatoka kwenye familia yenye changamoto ya kiuchumi kiasi cha kushindwa kumnunulia taulo za kike (sanitary pads). Kwa maelezo zaidi ya namna ya kuchangia tafadhali tupigie 0767666048
Ukifanikiwa katika kusudi la
maisha yako unakuwa maarufu pia kwenye maisha ya watu mbalimbali. Unapodhamiria kutimiza kusudi la maisha yako
ni vyema utambue kwanza umuhimu wa kufanikiwa kwenye maeneo mengine yanayogusa
maisha ya watu wengine.
Hakuna kusudi la maisha la
kutimiza pasipo kuona tatizo mahali fulani katika jamii inayokuzunguka. Hivyo
ni wajibu wako kuangalia jamii inayokuzunguka na kuangalia ni changamoto ipi
kati ya zilizoko katika jamii hiyo ambazo moyo wako unakusukuma kuitatua au
kuwa sehemu ya utatuzi. Mafanikio
yanaanza kwa kuitambua changamoto fulani kwenye jamii na kuitatua.
Changamoto ni nyingi kwenye
jamii zinazotuzunguka. Kwa mfano,
unaweza kukutana na mtu ambaye anatamani kufanya kile anachotakiwa kufanya
lakini hafanyi. Ni kitu gani unachoweza
kumfanyia au kumsaidia mtu kama huyu? Kitu kimoja wapo ni kutumia karama na vipawa
ambavyo MUNGU ameweka ndani yako kumsaidia huyu mtu kuziona fursa
zinazomzunguka ambazo zinamuwezesha kufanikiwa kwenye kile anachotaka kufanya;
lakini pia kumwezesha kuziona changamoto zilizokuwa zinamzuia yeye kufikia
lengo lake. Ukimsaidia kwa njia hii
unakuwa umegusa maisha yake kwa namna fulani.
Sio kila wakati tunahitaji kuwa
na pesa kuwasaidia watu kutoka kwenye changamoto zao.
Muhimu: Jitenge kutoka kwenye kundi la watu wanaoishi
maisha ya kawaida, maisha yasiyokuwa na athari yoyote au mguso wowote kwenye
jamii inayowazunguka. Hama kutoka kwenye
hayo maisha kwa kutumia kipawa na karama ulizo nazo. Kuwa mtu mwenye ushawishi kwenye jamii.
Ushawishi ni uwezo wa kuwafanya
watu wengine kukusikiliza au kufuatilia kile unachokifanya. Unakuwa mtu mwenye Ushawishi pale ambapo watu
wengine wanabadilisha vipaumbele vyao kwa ajili ya vipaumbele vyako.
Mafanikio yanakufanya uwe mtu
mwenye ushawishi katika jamii. Huwezi kufanikiwa
mpaka uwe na ushawishi na huwezi kuwa na ushawishi mpaka umefanikiwa. Vitu hivi vimeunganika na vinaambatana.
Ni nini asili ya mafanikio?
Tutaendelea wiki ijayo, usikose kutembelea ukurasa huu.
Imeandikwa na:
Lorna Dadi
http://lornadadi.com/wp-content/uploads/2017/02/ldf-logo.png00lornadfhttp://lornadadi.com/wp-content/uploads/2017/02/ldf-logo.pnglornadf2020-02-05 13:06:002020-02-05 13:06:08Mafanikio Yenye Ushawishi