Kwanini Huishi kwenye Kusudi la Maisha Yako?

Jaribu kufikiria jambo ambalo umekuwa ukitamani kulitimiza katika maisha yako lakini hujaweza kufanya hivyo.

Jambo ambalo lipo ndani kabisa ya moyo wako. Haijalishi ni kwa sababu gani hujaweza kulitimiza wewe litafakari tu.

Sio jambo la kushangaza, sisi wote nyakati flani katika maisha huwa tunateleza. Iko wazi tu hiyo. Wapo ambao wanaonekana kuwa bora kuliko sisi, hiyo ni kawaida tu kwani kuna ambao wanaonekana kutokuwa bora kama sisi.

Kwa kipindi ambacho nimekuwa nikijitolea kuzungumza na watu mbalimbali kuhusiana na changamoto wanazokutana nazo katika maisha, nimekuwa nikiulizwa ni changamoto gani kubwa ambayo nimeshakutana nayo katika maisha yangu. Huwa najitahidi kutokujibu hili swali kwani katika kila hatua ya maisha ninayopitia kuna changamoto zake.

Wengine wana matatizo ya mahusiano, wengine wana matatizo ya kifedha, wengine wana matatizo ya maradhi, nk Lakini tatizo kubwa nililokutana nalo kwa wengi wa hawa watu halikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na masuala ya mahusiano, pesa, maradhi au vinginevyo. Tatizo lipo kwenye kile mtu anachokiamini ndani ya nafsi yake.

Ni rahisi kujua namna ya kumtongoza mtu, ni rahisi kujifunza namna ya kuanzisha biashara, ni rahisi kujifunza namna ya kufanya kitu ambacho unaogopa. Lakini sio rahisi kumudu hali yako ya kutokujiamini, nk ni ngumu sana kumudu HALI iliyopo ndani yako. Kumudu hali yako ya ndani kunahitaji uwekezaji thabiti.

Nguvu nyingi unazoweka kwenye eneo fulani la maisha yako zinaathiri (hasi au chanya) maeneo mengine ya maisha yako. Kwa mfano, kama una tatizo la kutokujiamini, ukiweka nguvu nyingi kwenye kupambana na hali ya kutokujiamini, utaweza kubadilishi maeneo mengine mwengi ya maisha yako (athari chanya) kwa kuwa utakuwa na moyo wa kuthubutu. Kanuni yoyote ya maisha huwa haina ubaguzi, hivyo hata kanuni ya kushindwa kutokana na kutokujiamini pia haina ubaguzi. Kutokujiamini kwako kutasababisha wewe kushindwa katika maeneo mengine ya maisha yako. Fikra za aina fulani unazojijengea akilini mwako zinakwenda kuwa shina kwenye maeneo mengine ya maisha yako. Kuwa makini na aina ya Fikra unazoruhusu kubebwa na akili yako.

Hata Fursa katika maisha huja kulingana na ile hali iliyopo ndani yako – aina ya Fikra zilizopo kwenye akili yako, au niseme kiwango cha utayari kilichomo ndani yako. Unapokumbana na fursa ambayo wewe unajikuta umechagua kuiita kuwa ni kubwa, wengi wetu huwa tunazikwepa. Fursa kubwa za maisha huja katika hali ambazo hatukuzitegemea. Fursa zikija na sura ngumu, mara nyingi tunachoweza kufanya ni kutafuta sababu lukuki za kukwepa yale maumivu ambayo ni lazima tuyapitie ili tutimize ndoto zetu kupitia hizo fursa.

Zifuatazo ni mbinu kumi za Kushindwa kufanya jambo ninavyofikiria mimi. Tutaanza na zile nyepesi na kumalizia na nzito zaidi. Karibu sana.

1. Huna ujasiri wa kusimamia kile unachokiamini katikati ya watu wanaokuzunguka

Popote pale duniani Jamii kama Jamii ina nguvu ya asili ambayo haikubaliani na Mwanajamii yeyote anayeonyesha kujitambua na kujiamini kuliko Wanajamii wenzake. Hii ni nguvu ya asili. Watu hawapendi wanapoona mtu mwingine anabadilika au anafanya kitu kinachowafanya wao wajisikie wako chini au yule mtu anang’aa zaidi yao. Kujituma kwa bidii ili kufikia ndoto zetu au ukuu wa kusudi la maisha yetu huwa inasababisha wale wanaotuzunguka kujisikia kutokuwa wakamilifu. Na kutokujisikia kwao kuwa wakamilifu kunakuja kwa njia tofauti ila njia kubwa ni wivu na kutukatisha tamaa. Unapojituma kufikia ndoto yako maana yake ni kuwasha taa kwenye ndoto zao zilizofunikwa ndani ya boga – kitu kikiwa ndani ya boga hakiwezi kuona mwanga wa nje. Kwa kifupi hawa watu wanaumia kwenye fikra zao. Inawafanya wajihoji sana kuhusu wewe, jambo ambalo sio watu wengi wanaweza kulimudu kwani mtu anatakiwa ajihoji kuhusu yeye mwenyewe na sio ajihoji kuhusu mtu mwingine.

Ukweli mdogo kuhusu maisha: Ukitaka kufanya kitu fulani cha tofauti lakini chenye mantiki ndani ya moyo wako, ni lazima uridhike na hali ya kuwa tofauti na watu wengine katika hiyo jamii. Kuna wakati watafikiri umechanganyikiwa, mbinafsi, una dharau, mzembe, mjinga, huna nidhamu, nk. Wale ambao umekuwa ukiwaona na kuamini kwamba wako karibu na wewe ndio hao hao watakao kuwa mwiba kwako. Kama hujajizungushia wigo imara kwenye unachokiamini na kuamua kukifanya au hauna uhakika na mawazo yako na matamanio yako, basi huwezi kufika mbali kwenye jambo hilo.

2. Huna Dhamira ya kutosha

Mwaka 2009 mwandishi Karl Marlantes alifanikiwa kutoa kitabu chake kiitwacho Matterhorn, kitabu kinachoelezea uzoefu kwenye vita za Vietnam. Kitabu kiliuzwa sana. New York Times walikinukuu kama kitabu pekee kikubwa na cha kushangaza kilichowahi kuandikwa kuhusiana na habari za kivita.

Ilimchukua Bw. Marlantes zaidi ya miaka 35 hadi kitabu chake kuchapishwa – yaani zaidi ya nusu ya umri wake. Aliandika mswada wa hicho kitabu mara sita. Kwa miongo miwili hakuna kampuni ya uchapishaji iliyokubali miswada hiyo na wengi wa makampuni hayo hawakutaka hata kusoma hiyo miswada.

Wengi wengi mara nyingi huwa tunakata tama mapema sana kwenye masuala ambayo tunatamani kufanikisha katika maisha yetu. Lakini, mtu yeyote ambaye amefanikiwa kupitia njia halali ana mlolongo wake wa jitihada na changamoto.

Ukweli mdogo kuhusu maisha: Mafanikio mazuri na mafanikio yenye historia. Historia yeyote ina nyakati ngumu na nyakati nyepesi. Ukitaka kufanikiwa ni lazima uwe tayari kukabiliana na nyakati zote.

3. Huna Unyenyekevu

Kuna watu waliotuzunguka wanaweza kufanya jambo dogo sana kwa ukamilifu na jamii inaamua kuwaita watu hawa “Wataalamu”. Unyenyekevu ninaomaanisha hapa ni kujua kile usichokijua

Katika ulimwengu wa biashara za mtandaoni, nimejifunza vitu vingi sana. Watu ambao wamekuwa waongeaji wazuri kuhusu mafanikio na wakati mwingine wakayakuza na hivyo kupata wafuasi wengi – wachache wana mafanikio ya wastani tu. Na wakati wengine hawajafanikiwa kabisa! Wengine bado ni tegemezi kwa watu wengine! Lakini bado wako radhi kujitapa kwa yeyote ambaye yupo tayari kuwasikiliza.

Lakini watu ambao wana utajiri halisi, utajiri uliotokana na kufanya kazi kwa bidii, utajiri uliopitia nyakati ngumu na nyepesi; ni mara chache sana kuwakuta wakiwa wanaongea ongea sana kuhusu kufanikiwa kwao, mara nyingi hupenda kuongelea kuhusu changamoto walinazokutana nazo katika mafanikio yao na jinsi gani walihitaji kujifunza zaidi kutokana na changamoto hizo.

Ukweli mdogo kuhusu maisha: Safari ya mafanikio inaambatana na changamoto nyingi, hizi changamoto unatakiwa uzione kama fursa ya kujifunza vile vitu ambavyo ulikuwa huvijui kwa sababu unataka kupata kitu ambacho ulikuwa huna ni lazima ujifunze vitu vipya vinavyoendana na hicho kitu ambacho unakitaka.

 

……… Tutaendelea namba 4-10 ………